May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

PSSSF yapewa tuzo kimataifa

 

NA K-VIS BLOG/KHALFAN SAID, DAR ES SALAAM

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umepewa tuzo na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA)kutokana na mafanikio iliyoyapata katika kipindi kifupi baada ya kuunganishwa (Merge) kwa mifuko minne ya Hifadhi ya Jamii ya PSPF, PPF, GEPF NA LAPF na kuwa PSSSF.

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba alisema sababu nyingine iliyoifanya ISSA kutoa tuzo kwa Mfuko huo ni pamoja na jinsi Mfuko ulivyoweza kupunguza gharama za uendeshaji na ulipaji wa mafao kwa wakati.

“Kwenye suala la kuunganisha mifuko yapo mambo manne ambayo ISSA imeyaona na kuona ni mafanikio ambayo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kutoa mafao yanayofanana kwa wanachama wa Mfuko licha ya kutoka kwenye mifuko tofauti, kukabiliana na madeni kabla ya mifuko kuunganishwa na pia suala la uwekezaji hususan katika viwanda.” Alisema

CPA Kashimba aliishukuru Bodi ya Wadhamini kwa usimamizi mzuri na hivyo kuufanya Mfuko huo kufanya vizuri.

“Kazi kubwa ya kusimamia zoezi hili la kuunganisha mifuko mmeifanya ninyi Bodi kwa maelekezo ya serikali, sehemu nyingi duniani wanasema karibu asilimia 85 ya kampuni zilizoungana huwa zinashindwa lakini muunganiko wetu sisi umeendelea kufanya vizuri hadi kuivutia taasisi hii kubwa kuifanya PSSSF kuwa mfano wa kuigwa.” Alisema CPA Kashimba.

Alisema tayari Mfuko umeanza kupokea wageni KUTOKA sehemu mbalimbali wakihitaji kujifunza kutoka PSSSF.

“Juzi kamati ya bunge ya Uganda wao wanaanzisha Mfuko wa Watumishi wa Umma na walikuja kujifunza na wameridhishwa na elimu tuliyowapatia.” Alifafanua.

Alisema tuzo hiyo ni zawadi kwa Bodi na sio Menejimenti pekee na mfuko uko kwenye mikakati ya kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora kwa Wanachama na Wastaafu kwa ujumla.

Awali Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa alidokeza kuwa eneo lingine ambalo liliwavutia watoa tuzo ni jinsi mfukoulivyofanya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma kwa wastaafu na wanachama. 

“Suala la Huduma kwa wananchama, jinsi tunavyokusanya michango, tunavyolipa mafao, kutoka kwenye matumizi ya hundi kulipa mafao, lakini jinsi tunavyohakiki wastaafu wetu, haya yote yaliwavutia.” Alifafanua Bw. Magawa.

Aidha Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma (PSSSF) Bw. James Mlowe alisema PSSSF ilikabidhiwa tuzo hiyo jijini Abidjan Ivory Coast Mei 17, 2023 na kwamba ifikapo Agosti Mosi, 2023 PSSSF itafikisha miaka mitano tangu kuundwa kwake baada ya kuunganishwa kwa mifuko (merge), Agosti Mosi, 2018.

“Majukumu ya mfuko yanatekelezwa vizuri, uwezo wa mfuko unazidi kuimarika, watumishi wanazidi kuwa kitu kimoja na kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kwakweli mafanikio haya ndiyo yamewavutia ISSA kuweza kutoa tuzo hii” Alisema

“Tunajisikia faraja kwa tuzo hii na hii imekuwa chachu ya  kuendelea kutekeleza majukumu yetu sawasawa kuendelea kuwahudumia wanachama wetu na wastaafu kikamilifu.” Alitoa hakikisho.

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF),  Dkt. Aggrey Mlimuka (kulia) akipokea tuzo ya Kimataifa inayotolewa na Taasisi ya Kimataifa ya Hifadhi ya Jamii (International Social Security Association-ISSA) kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA. Hosea Kashimba katika hafla fupi iliyofanyika Makao Makuu ndogo ya PSSSF jijini Dar es Salaam Mei 30, 2023. PSSSF ilipewa tuzo hiyo na ISSA kwa kutambua mafanikio iliyopata PSSSF katika kipindi kifupi ndani ya muundo mpya wa mifuko kuunganishwa (merging).

Mkurugenzi wa Uendeshaji PSSSF, Bw. Mbarouk Magawa, akielezea mchakato uliopelekea PSSSF kupewa tuzo hiyo.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma PSSSF, Bw. James Mlowe, akionesha tuzo hiyo.