May 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman mgeni rasmi mkutano wa EAPC

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Othman Masoud Othman anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika Mkutano wa Nane wa Uhisani Afrika Mashariki (EAPC) utakaofanyika Visiwani Zanzibar kuanzia tarehe 28 mpaka 30 Juni, 2023 katika Ukumbi wa Madinat Al Bahr Hotel.

Mkutano huu ulioandaliwa na Mtandao wa Uhisani Afrika Mashariki (EAPN) pamoja na Legal Services Facility (LSF) utajumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya uhisani ikiwemo wahisani, wajasiriamali, viongozi kutoka sekta binafsi pamoja na watunga sera kwa ajili ya kutathmini na kujadili changamoto zilizopo katika sekta ya uhisani chini ya kauli mbiu inayosema ‘Mabadiliko ya Mifumo: Kuhamasisha Jitihada za Pamoja.’

Akizungumza na waandishi wa Habari leo, Afisa Mtendaji wa EAPN, Evans Okinyi amesema Uwepo wa Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Othman Masoud Othman katika mkutano huo unaongeza umuhimu wa mkutano huo, ukirejelea kujitolea kwa serikali katika sekta ya uhisani ili kusukuma maendeleo endelevu katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ni fahari kubwa kuwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, akiwa kama Mgeni Rasmi katika mkutano wetu. EAPN tunaamini uongozi wake wa kipekee na dhamira yake isiyoyumba ya kupigania ustawi wa jamii na maendeleo endelevu itaongeza hamasa ndani ya kila mshiriki, hivyo kuchochea majawabu ya changamoto zinazoikabili jamii yetu. Uwepo wake ni hatua muhimu kuhamasisha mbadiliko ya mifumo na sera ili kuunda mustakabali wa sekta ya uhisani ambayo ni endelevu katika ukanda wetu,” ameeleza Afisa Mtendaji wa EAPN, Evans Okinyi.

“Katika Mkutano huo inatarajiwa kuwa washiriki wa mkutano watakusanyika kutoka sekta mbalimbali huku wakiangazia masuala muhimu kupitia utaalamu wao kama sehemu ya jukwaa muhimu la ushirikiano miongoni mwa wadau ili kuleta mabadiliko. Pia, washiriki wataweza kushuhudia matokeo muhimu ya sekta ya uhisani kwenye jamii, hususani katika kuchangia maendeleo yenye tija.”

Mkutano wa Nane wa Uhisani Afrika Mashariki unakusudia kuleta uzoefu wa kina miongoni mwa washiriki kupitia uwasilishaji wa hotuba mbalimbali, mijadala, pamoja na kuongeza wigo wa fursa za ushirikiano miongoni mwa wadau hivyo EAPN na LSF imewakaribisha wahisani, wajasiriamali, viongozi kutoka sekta binafsi, watunga sera, na mabalozi wote wa maendeleo endelevu kote Afrika Mashariki kuchangamkia fursa hiyo ili kujadili masuala ya maendeleo.