May 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof:Makubi awaondoa hofu Watanzania kuhusiana na Corona

Judith Ferdinand,TimesMajira online,Mwanza

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi amewaondoa hofu Watanzania,wageni pamoja na watalii juu ya ugonjwa wa corona(COVID-19) huku akiwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi(kulia) akiwa na Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Dkt.Thomas Rutachunzibwa( kushoto) wakati alipo tembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou -Toure ambapo alipata fursa ya kukagua idara mbalimbali ikiwemo chumba cha CT-Scan pamoja na kuzungumza na wagonjwa walikuwa wakipata matibabu katika hospitali hiyo.Picha zote na Judith Ferdinand

Prof.Makubi ameyasema hayo wakati alipotembelea hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou -Toure ambapo alipata fursa ya kukagua idara mbalimbali ikiwemo chumba cha CT-Scan pamoja na kuzungumza na wagonjwa walikuwa wakipata matibabu katika hospitali hiyo.

Wasafiri pamoja na watalii wanaweza kuja nchini bila wasiwasi lakini kuna utaratibu wanapewa huku Watanzania wakiendelea kuchukua tahadhari zote za kujikinga ili udhibiti uliopo sasa uendele zaidi na ndio suala la msingi ambalo anawaomba wananchi waendelee kukaza na wasilegeze kamba katika kutii maelekezo ya kuchukua tahadhari zote dhidi ya corona.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi akizungumza na baadhi ya wagonjwa

Amesema Serikali imeendelea kudhibiti tatizo la COVID-19 mpaka sasa hivyo amewadhibitishia wananchi kuwa taifa lipo katika hali nzuri na wasiwe na hofu.

Pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan,ameweka mfumo mzuri wa kushughulikia suala hili na mpaka sasa hivi wanaweza kuona udhibiti zaidi pengine kuliko hata mwaka jana.

“Sisi kama Wizara tunaona tupo kwenye hali nzuri,sasa hivi tumeidhibiti sana COVID-19 pengine kuliko nchi yoyote ile,na jitihada hizi zilianza kuanzia mwaka jana kwenye Serikali ya awamu ya tano na zimepokelewa na kuendelezwa vizuri na Serikali hii ya awamu ya sita,” amesema Prof.Makubi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi wa tatu kushoto akiangalia mashine ya CT-Scan

Hata hivyo amesema,anachopaswa kufanywa na wananchi kwa sasa ni kuhakikisha wanatii maelekezo yanayotolewa na wataalamu kwani amepita katika hospitali hiyo ya Sekou- Tou’re amekuta miundombinu mizuri imewekwa ya kujikinga na COVID-19 ikiwemo sehemu za kunawia mikono na watoa huduma wanavaa barakoa kwani ni eneo ambalo lina hatari kubwa hivyo lazima wajikinge na kuchukua tahadhari zote.

Kwa hiyo Watanzania waendelee kuchukua tahadhari za kunawa mikono na kuvaa barakoa hususani zilizotengezwa nchini hapa na MSD zenye ubora unaotakiwa.

“Niwaambie Watanzania wote na wasafiri kuwa wasiwe na hofu yoyote cha msingi ambacho ni waombe wananchi ni waendelee kuchukua tahadhari kwani awali wameweza kuchukua tahadhari vizuri sana na ndio maana tumeweza kudhibiti ,niendelee kuwapongeza Watanzania kwa sababu haya ni matunda ya wao kuwa wasikuvuu,”amesema Prof.Makubi.

Aidha amesema,tofauti na kunawa mikono na kuvaa barakoa pia kuna njia nyingine ya kujingika na COVID-19 ambazo ni pamoja na kupunguza misongamano isiyokuwa ya lazima.

Pia kufanya mazoezi kwani ugonjwa huu unathiri sana watu ambao wana magonjwa ambayo siyo ya kuambukiza kama kisukari,shinikizo la damu na moyo.

Pamoja na kuzingatia lishe bora ambayo inasaidia kinga za mwili kama matunda pia kumekuwa na tiba za asili ambazo nazo zinapaswa kuendelea kuhamasishwa na wakiendelea kuzingatia hayo yote ugonjwa huo wataendelea kuudhibiti na pengine kuudhibiti zaidi hivyo hakuna haja ya watu kuwa na hofu.

“Tunapo fanya mazoezi inasaidia,tumeona wana michezo wengi wameweza kupata ugonjwa huu katika nchi zilizoendelea lakini sijasikia kifo wengi wameweza kuudhibiti kwa kutumia kinga ya mwili wao na baadae ugonjwa unaisha,hivyo mazoezi tuendelee kuyafanya angalau mara tatu au nne kwa siku kwa nusu saa hadi mwili utoe jasho pia tuzingatie lishe,”amesema Prof.Makubi.