May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof. Ndalichako: Fao la huduma ya utengemao kuongeza faraja

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

SERIKALI kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanmyakazi (WCF) imetangaza Fao jipya la Huduma ya Utengemao wa Kijamii (Social Rehabilitation) kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi na hivyo litawaongezea faraja, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, amesema.

Akizungumza jijini Dar es Salaam,  Novemba 29, 2023, alipokutana na wanufaika wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani inayotarajiwa kufanyika kitaifa jijini Dodoma, Desemba 2, 2023. 

Profesa Ndalichako mesema, “Ndugu zangu hivi karibuni tutaanza kutoa Fao la Huduma ya Utengamao wa Kijamii na kutoa mafunzo ya kujenga ujuzi kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu wakiwa kazini na aina ya ujuzi tutakaotoa utategemea uhitaji.” Alisema

Alisema lengo la Serikali ni kumpatia mfanyakazi ujuzi ambao utaendana na hali ya ulemavu wake, mfano alikuwa dereva na akapata ajali iliyopelekea ulemavu wa miguu, huyu anaweza kubadilisha ujuzi na kusomea kazi nyingine. 

Sambamba na kuwajengea ujuzi, fao hilo pia litatoa fursa ya kumjengea miundombinu inayoendana na hali yake, na hivyo kumuwezesha kumudu maisha katika mazingira anayoishi.” Alifafanua Profesa Ndalichako.

Kwa upande wao, wanufaika wa WCF wameishukuru Serikali kwa huduma wanazopokea kutoka katika Mfuko huo licha ya kupata ulemavu na wengine kuondokewa na wapendwa wao.

“Naomba kuhamasisha waajiri kuweza kuwachangia wafanyakazi wao, kwani viwango vya uchangiaji ni vidogo, tunaishukuru Serikali imepunguza viwango vya uchangiaji hadi kufikia asilimia 0.5” Alisema Norbert Tesha, ambaye amepata ulemavu wa kudumu baada ya kupata ajali akiwa kazini mwaka 2016.

“Hatuwezi kujua kesho yetu, lakini kama kuna misingi mizuri iliyowekwa leo, basi kesho yetu itakuwa njema, kila mtu ni mlemavu mtarajiwa.” Alisema, Bw. Tesha.

Mnufaika mwingine Bi. Emmaculet Nhigula, ambaye alimpoteza mumewe kwa ajali ya gari, amesema, “Mimi na watoto wangu wanne, tunanufaika sana na Mfuko huu, rafiki yetu kwa sasa ni WCF, huwa nikipita kwenye barabra hii na kuliona jengo lenu, ninasema hawa ni rafiki zangu wanaotembea na mimi nyakazi ngumu.” Alisema

Alisema yale mafao ya kila mwezi yamekuwa na msaada mkubwa sana, yamesaidia kusomesha watoto wangu na sikuweza kuwahamisha kutoka shule walizokuwa wanasoma kabla ya kufariki baba yao.” Alisema Bi. Emaculate. 

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu, yanalenga kuwahamasisha viongozi wa taasisi za kibiashara Duniani kutambua mchango maridhawa wa watu wenye ulemavu.

Kwamujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kwasasa inakadiriwa kuwa watu bilioni 1.3 duniani wanaishi na changamoto ya ulemavu, hii ni sawa na asilimia 16% ya Watu wote duniani.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “ Tuungane katika hatua za Kuokoa na kufikia Malengo ya SDGs kwa Watu wenye Ulemavu”.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako (wapili kushoto) akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma (wakwanza kushoto), wakati akizungumza na wanufaika wa Fidia inayotolewa na WCF, kwenye Ofisi za Mfuko huo, jijini Dar es Salaam. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako akizunguzma kwenye mkutano na waandishi w ahabari jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza kwenye mkutano na waandishi w ahabari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma.

 Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, akizungumza mwanzoni mwa mkutano huo.

Bw. Norbert Tesha (kushoto), Mnufaika wa WCF, akitoa ushuhuda mbele ya waandishi wa habari jinsi anavyonufaika baada ya kupata ulemavu wa kudumu kufuatia kuumia katika ajali iliyotokana na kazi

Bw. Kelvin Cameroon,  mnufaika wa WCF, akitoa ushuhuda mbele ya waandishi wa habari jinsi anavyonufaika baada ya kupata ulemavu wa kudumu kufuatia kuumia katika ajali iliyotokana na kazi

Bi. Emmaculat Nzigula, Mtegemezi anayenufaika na mafao yanayotolewa na WCF baada ya kumpoteza mumewe aliyefariki katika ajali ya gari wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri wake.

Profesa Ndalichako, akisalimiana na mmoja wa wategemezi wanaonufaika na mafao ya Fidia. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF.

Profesa Ndalichako, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za WCF jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma na Bw. Rasheed Maftah, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma kwa  Wenye Ulemavu, Ofisi ya Waziri Mkuu.

Picha ya pamoja.