Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Mwanza
JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza linafanya uchunguzi kufuatia kifo cha mwanafunzi Stellah Shilingi(15),aliyekuwa akisoma kidato cha tatu, mkondo B, katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Loreto anayedaiwa kujirusha kutoka juu ya ghorofa ya kwanza hadi chini.
Akizungumza Septemba Mosi,2026 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbord Mutafungwa alisema,tukio hilo lilitokea Agosti 31,2026 majira ya saa 11:00 asubuhi katika Mtaa wa Majengo Mapya, Kata ya Nyakato wilayani Ilemela mkoani humo.
Ambapo inadaiwa mwanafunzi huyo akiwa na wanafunzi wenzake wakielekea kufanya usafi shuleni hapo, alijirusha kutoka juu ya ghorofa ya kwanza hadi chini na kupata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.
DCP.Mutafungwa amesema,mara baada ya tukio hilo, alipata msaada wa haraka kwakuchukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya matibabu.Lakini baada ya kufikishwa hospitalini hapo ilibainika kuwa tayari amekwisha fariki.
Uchunguzi wa awali unaonesha chanzo cha tukio hili ni msongo wa mawazo wa muda mrefu uliotokana na ugomvi wa kifamilia kati yake na mama yake mzazi.
“Kutokana na taarifa za awali zimebainisha kiwa binti huyo akiwa likizo ya mwezi wa sita mwaka 2026 nyumbani kwao anakoishi na mama yake, alijaribu kujiua kwa kumeza vidonge lakini aliokolewa na mama yake pamoja na ndugu wengine.Pia hata shuleni imebainika amekuwa na tabia ya kujitenga na kabla ya kujirusha hhorofani aliacha ujumbe wa maandishi akieleza dhamira yake ya kutaka kujiua,”amesema DCP.Mutafungwa.
Hata hivyo ametoa pole kwa familia, ndugu,wanafunzi wenzake na uongozi wa shule kwa msiba huo.
“Wakati uchunguzi ukiendelea,natoa wito kwa wazazi,walezi na viongozi wa taasisi mbalimbali kuimarisha mifumo ya ushauri nasaha na malezi ya karibu ili kuwatambua na kuwasaidia mapema vijana wanaokabiliwa na changamoto za kisaikolojia,”amesema DCP.Mutafungwa.
Vilevile amesema,jeshi hilo linaendelea kutoa elimu kwa wazazi,walimu na watu wengine wenye nafasi kwenye jamii kuhakikisha kwamba wanasikiliza matatizo au changamoyo za watoto na kuzifanyia kazi mapema kabla watoto hao hawajachukua maamuzi hayo mazito ya kukatisha uhai wao.

More Stories
Yas yatambulisha uzi mpya wa Zanzibar Marathon
Ilemela yatakiwa kusimamia mifumo ukusanyaji mapato
Msigwa:Usikubali kumsajilia mtu laini ya simu