May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Polisi wachunguza kifo cha mwanafunzi aliyekula sumu

Na Judith Ferdinand, TimesMajira, Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza uchunguza kifo cha mwanafunzi pamoja na watu wengine 18 walioathirika kwa kile kinachodaiwa kula chakula chenye sumu Wilayani Sengerema Mkoani hapa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Muliro Jumanne amesema, Agosti 24 mwaka huu saa 10 jioni katika kituo cha afya Mwangika Kata ya Bangwe Wilaya ya Sengerema Mkoani hapa, Mboni Mahano ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Mwangika, alifariki wakati akipatiwa matibabu katika kituo hicho baada ya kudaiwa kula chakula kinachodaiwa kuwa na sumu alipokuwa kwenye sherehe.

Amesema, mwili wa marehemu umeifadhiwa kituo cha afya Mwangika kwa uchunguzi wa daktari huku ule wa awali ukibaini kuwa Agosti 22 mwaka huu kulikuwa na harusi nyumbani kwa Dorica Omajigo.

Agosti 23, mwaka huu wanawake mmoja na watoto wao walirudi kusafisha vyombo ndipo wakala tena chakula kilichobaki na baada ya masaa kadhaa walianza kuumwa na kukimbizwa katika kituo cha afya cha Mwangika ambapo kati yao 18 (watu wazima wanne na watoto 14) wamelazwa kwa matibabu.

Aidha amesema, jeshi hilo linafuatilia kwa karibu tukio hilo na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika na kitendo hicho.