April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Martin Gugino, Mzee aliyesukumwa na askari polisi wakati wa maandamano na kuangukia kichwa na kutokwa na damu

Polisi Marekani wajiuzulu wote kwa tukio la mzee wa miaka 75 kuangushwa wakati wa maandamano

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Kitengo chote cha Idara ya Polisi wa Buffalo mjini Albany, New York Marekani kimejiuzulu kutekeleza wajibu wao baada ya maofisa wawili wa jeshi hilo la polisi kupumzishwa, baada ya kilio cha wananchi kuhusiana na video iliyosambaa ikionesha maofisa hao wakimsukuma mzee wa miaka 75 na kudondoka chini, hivyo kuumia kichwani.

Askari polisi wakimsukuma Mzee Martin Gugino (75)

Kwa mujibu wa kituo cha Buffalo News na vyombo vingine vya habari jijini New York, askari polisi wote 57 wa kitengo hicho cha dharura wamejiuzulu katika kitengo hicho, wafanyakazi wa kitengo hicho cha polisi cha miito ya dharura hawajaacha kazi ya upolisi, lakini wamejitoa katika kitengo hicho maalum.

Mwanasheria Kelly Zarcone alitoa taarifa kuwa, Martin Gugino, mzee aliyesukumwa na kuangukia kichwa ni mwandamanaji wa amani kwa muda mrefu, mtetezi wa amani na mtetezi mkubwa wa Katiba ya nchi ya Marekani.

“Gugino anumwa sana japo hali yake bado iko sawa. Anajitambua na kuelewa mambo yanayoendelea,”imeeleza taarifa ya Zarcone iliyotumwa kwa njia ya barua pepe. Ameomba faragha na kwamba katika maandamano yajayo yawe ya amani.

Video iliyosambaa mitandaoni iliwaonesha maofisa wa jeshi la polisi wakimsukuma Gugino na kuanguka chini alipowasogelea askari hao katika eneo la maandamano siku ya Alhamisi saa nane mchana. Gugino alianguka chini na kupoteza fahamu huku akitokwa na damu kichwani.

“Tunatambua kuwa hawa polisi walikuwa wanatekeleza amri kutoka kwa Kamishna wa Polisi, Joseph Gramaglia ya kutawanya waandamanaji katika eneo hilo,”alisema kiongozi wa umoja wa polisi wa Idara ya Polisi Buffalo, John Evans.

“Amri haielezi kwamba tuachane na wenye umri zaidi au chini ya miaka 50 au miaka 15 mpaka 40. Walikuwa wanafanya kazi yao, sijui walitumia nguvu kiasi gani, kwa mtazamo wangu aliteleza tu na kuangukia nyuma,” ameeleza Evans alipoulizwa kuhusu maofisa waliojiuzulu katika mkutano na wanahabari, Mkurugenzi wa eneo la Erie, Mark Poloncarz amesema inakatisha tamaa kama kweli wamejiuzulu.

“Kama wamejiuzulu, binafsi nimesikitishwa na hatua hiyo sababu inaonesha wazi hawakuona tatizo lolote kwa kitendo hicho,”ameeleza Poloncarz.

Maoni yametolewa dhidi ya tukio hilo na wananchi na viongozi mbalimbali hata hivyo kitengo cha Mwanasheria wa Ofisi ya Wilaya ya Erie aliandika katika mtandao wa Twitter kuwa, bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la kusukumwa mzee huyo wa miaka 75 na kwamba hawakutoa maelezo yoyote.

Kitendo cha maofisa hao wa polisi kilizua taaruki na manung’uniko nchi nzima, ambapo pia Meya wa New York, Andrew Cuomo ameeleza kuwa, “kitendo hicho hakifai na ni cha kulaaniwa”.

Katika mkutano na waandishi wa habari Cuomo alionesha video ya tukio lile ili angaliwe kwa makini kabla ya kuwahoji maofisa husika.“Unaona katika video na inasumbua hata ukiitazama kibinadamu,”amesema Cuomo.