July 3, 2022

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pinda : Wadau wa msaada wa kisheria imarisheni ushirikiano na Serikali

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala akizungumza na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria nchini (hawapo pichani) wakati wa kufunga Kongamano la Msaada wa Kisheria 2022 lililofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma.

NAIBU Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Geofrey Pinda amewataka wadau wa msaada wa kisheria nchini kujenga na kuimarisha ushirikiano ya kimkakati na serikali ikiwa ni fursa ya kuwasilisha mapendekezo yenye tija kwa lengo la kuboresha sekta ya msaada wa kisheria nchini.

Waziri Pinda aliyasema hayo mwishoni mwa juma lililopita wakati wa kufunga kongamano la siku mbili Jijini Dodoma lililowakutanisha wadau wa sekta ya msaada wa kisheria takribani 120 kutoka Tanzania bara na visiwani kwa lengo la kutathimini utekelezaji wa Sheria ya Msaada wa Kisheria ya Mwaka 2017 pamoja na kuangalia huduma ya msaada wa kisheria kwa ujumla.

Alisema kuwa serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria ni wadau muhimu katika utendaji kazi hasa katika sera, sheria, masuala mbalimbali ya haki ambayo yanawahusu wananchi.

Mratibu wa Mtandao wa Watoa huduma za Msaada wa Kisheria na Wasaidizi wa Kisheria nchini (Tanzania Paralegals Network – TAPANET), Tolbert Mmasy, akisoma hotuba fupi kuhusu masuala mbalimbali yaliyoazimiwa na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria mbele ya Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nchini, Geofrey Pinda, wakati wa kufunga Kongamano la Msaada wa Kisheria 2022 lililofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma.

“Ninaamini kwamba ili kuwepo matunda mazuri, kunahitajika uhusiano endelevu kati ya serikali na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria.

“Kwa kutambua hilo, nawahakikishia kuwa ofisi yangu itakuwa wazi kufanya kazi na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria kwa kupokea taarifa, ushauri na mazungumzo mengine muhimu kuhusu mambo mbalimbali yanayowakabili wananchi katika sekta hii nyeti nchini,” alisema.

Waziri huyo aliongeza kuwa Serikali iko tayari kufanya kazi na wadau wa sekta ya msaada wa kisheria katika mazingira rafiki, huru, uwazi na usawa ili kusukuma mbele maendeleo ya sekta ya msaada wa kisheria kwa kuwa lengo ni kujenga nchi moja.

Aidha, Naibu Waziri Pinda, aliwapongeza watoa huduma za msaada wa kisheria kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii kwa kujitolea kwa lengo la kuwezesha jamii hususani wale wasio na uwezo wa kupata huduma za msaada wa kisheria kupata usaidizi na utatuzi wa changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo.

Msaidizi wa Kisheria kutoka Shirika la Msaada wa Kisheria Wilaya ya Kinondoni, Anthony Isakwi, akitoa mapendekezo yake namna ya kuboresha zaidi sekta ya msaada wa kisheria wakati wa kufunga Kongamano la Msaada wa Kisheria 2022 lililofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma.

“Ni muhimu sisi kama Wizara ni kutathimini thamani ya utoaji wa msaada wa kisheria na kuimarisha huduma za msaada wa kisheria nchini kwa kujengea uwezo watoa huduma wa msaada wa kisheria.

“Na ndio maana sisi kama Wizara tukaona ni vyema kuondoa vikwazo kama vile ada ya mwaka kwa wasaidizi wanaojitolea bila malipo yoyote na kuendelea kuboresha huduma hizi nchini“ alisema.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala, ambao ndio waandaaji wa kongamano hilo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, alisema kuwa kongamano hilo la siku mbili lilijadili kwa kina masuala mbalimbali na kuibuka na maazimio ambayo baadae kikosi kazi cha wadau kitaandaa ripoti na kuiwasilisha serikali kwa ajili ya utekelezaji zaidi.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala (kushoto) akisalimiana na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nchini, Geofrey Pinda, mara baada ya kuwasili kwenye Kongamano la Msaada wa Kisheria 2022 akiwa kama Mgeni Rasmi kwa ajili ya shughuli ya kufunga kongamano hilo lililofanyika hivi karibuni Jijini Dodoma.

“Kikao hiki kimetupa maazimio mengi. Niahidi kuwa, wataalamu wetu wamerekodi yote yaliyojadiliwa na wadau. Baada ya kongamano hili timu hiyo itaandaa taarifa rasmi kwa ajili ya kuiwasilisha serikalini ili ifanyiwe kazi kwa ajili ya kuboresha na kuongeza ufanisi wa sekta ya msaada wa kisheria nchini” alisema Ng’wanakilala.

Vilevile, Ng’wanakilala aliishukuru Serikali chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha inatoa mafunzo kwa watoa huduma za msaada wa kisheria na kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma hizi kwa wanawake na watoto, ambao ndio wahanga wakubwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Akisoma hotuba fupi kuhusu masuala mbalimbali yaliyoazimiwa katika kongamano hilo, Mratibu wa Mtandao wa Watoa huduma za msaada wa kisheria na wasaidizi wa kisheria nchini (TAPANET), Tolbert Mmassy, aliipongeza serikali kwa kuondoa ada ya usajili kwa watoa huduma za msaada wa kisheria, hali itakayoongeza idadi ya wadau wanaojisajili katika mfumo wa serikali na kutambulika kisheria.

Katika picha ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria nchini Tanzania, Geofrey Pinda (katikati) na Katibu Mkuu Wizara hiyo, Mary G. Makondo. Wengine Msajili wa Huduma za Msaada wa Kisheria, Felistas Mushi (wa kwanza kushoto), Afisa Mtendaji wa Shirika la Legal Services Facility (LSF), Lulu Ng’wanakilala (wa pili kulia) na Mrajisi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali Zanzibar, Ahmed Khalid, wakati wa kufunga Kongamano la Msaada wa Kisheria 2022 hivi karibuni Jijini Dodoma.

Pamoja na hayo wadau wa kongamno hilo waliazimia mambo mbalimbali ambayo yanahitaji kuboresha sekta ya msaada wa kisheria ikiwemo; kutambulika kwa wasaidizi wa kisheria kila ngazi ili waweze kuwahudumia wananchi, watoa huduma za msaada wa kisheria kupewa ofisi katika majengo ya umma ili kuwasaidia watu wengi zaidi wenye uhitaji, utekelezaji wa shughuli za huduma za msaada wa kisheria kwa kushirikiana na serikali ili kuongeza wigo wa huduma za msaada wa kisheria kwa wadau mbalimbali,watoa huduma za msaada wa kisheria kujengewa uwezo kwenye mifumo na sheria jinai pamoja na kuiomba serikali kutenga ruzuku maalumu katika kutoa msaada wa kisheria ili kuhakikisha kuwa huduma hizi zinakuwa endelevu.