May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya Wanasheria wakiangalia na kujadiliana kwa kina sheria ya matumizi ya mtandao.

Paradigm Initiative Afrika yawakutanisha wadau kujadili sheria ya matumizi ya mtandao

Na Penina Malundo,TimesMajira,Online

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Paradigm Initiative Afrika limewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria na waandishi wa habari kwa lengo la kujadili sheria ya matumizi ya mtandao na haki za mtumiaji kuendana na uhitaji wa sasa na baadae.

Majadiliano hayo ambayo yamefanyika kwa siku mbili kwa njia ya mtandao yalihusisha pia wadau kutoka nchi ya Nigeria ambapo kwa pamoja walitoa maoni yao na kuomba kupata uzoefu kutoka Tanzania ambayo tayari imepiga hatua ikiwemo kudhibiti kikamilifu matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Pamoja na mambo mengine wadau wamepata nafasi ya kuangalia na kujadili muswada wa Nigeria unaohusu masuala ya matumizi ya mtandao pamoja na kuangalia ni maeneo gani ya kusaidia kuboresha ufanisi, misingi bora ya utumiaji ya mitandao ya kijamii kwa Tanzania na Afrika ya sasa kwa siku za baadae.

Akizungumza kuhusu majadiliano hayo Mdau na mtumiaji wa mtandao, Mratibu wa majadiliano hayo, Peter Mmbando amesema watumiaji wa mtandao ya kijamii wanapaswa kuitumia kwa usahihi hasa kwa kufuata sheria.

Hata hivyo Mmbando amesema kwamba ni wakati mwakafa wa kubadilishana uzoefu kati ya Tanzania na nchi nyingine ikiwamo Nigeria ili kuona nini cha kujifunza kuendana na wakati kwa mahitaji ya sasa na baadae.

“Nawaomba watumiaji wa mtandao tuendelee kufuata sheria zilizopo ili kuendana na mahitaji ya sasa na baadae lakini kama kutakuwa na maboresho tufikishe maoni yetu kwenye vyombo husika kwa ajili ya kujadili na kujenga hoja,” amesema Mmbando

Ameongeza washiriki wametoa maoni yao kulingana na muktadha wa nchi yetu na nchi nyingine za Afrika kama bara moja ambalo linatamani kuwa na maudhui yanayoendana na Waafrika katika kutumia intanenti.