May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Pandahill waishukuru serikali kupatikana kwa mwanafunzi Ester

Na Esther Macha, Timesmajira, Online,Mbeya

UONGOZI wa shule ya sekondari Pandahill ukiongozwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Mbeya,Gervas Nyaisonga umeishukuru serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kupatikana kwa mwanafunzi wa shule hiyo Ester Noah Mwanyilu (18)aliyetoweka Mei 18 na kupatikana Juni 23 mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Juni 29,2023 kwa niaba ya Mhashamu Baba Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga ,Mkuu wa shule ya sekondari ya Pandahill ,Zephania Lusanika amesema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo ni Kamati ya Ulinzi na Usalama za Wilaya chini ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera vilihakikisha vinakuwa bega kwa bega na shule hiyo katika kipindi chote cha kumtafuta Mwanafunzi huyo.

Pia Mkuu huyo wa shule amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa kuonesha ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwezesha kupatikana kwake Mwanafunzi Ester.

“Nitoe rai kwa wazazi, walezi kuwaongoza watoto kwa kufuata misingi ya sheria,dini,maadili, nidhamu na haki ili waweze kupambana na changamoto za maisha popote wanapokuwa lakini kwa wanafunzi waendelee kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na shule ili kurahisisha usimamiaji na ufuatiliji wa nidhamu shuleni”amesema. Mkuu wa Shule Lusanika.

Lusanika amitaka jamii iendelee kuviamini vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano wa taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo ili uchunguzi uweze kufanyika kwa haraka, uhuru na haki na endapo itabainika mtu au watu kuhusika na tukio hilo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Akizungumzia kuhusu nidhamu ya Shule ,Lusanika amesema kuwa Shule imejengwa kwa misingi ya kufuata sheria,kanuni na taratibu za nchi na kanisa kuhakikisha Mwanafunzi awapo shuleni awe mwenyewe upendo,mtiifu kwa wakubwa na mamlaka za nchi,mwaminifu,mcha Mungu mwenye kujitambua na mwenye tabia njema inayokubalika na jamii.

“Tunatoa ahadi kwa jamii kuwa shule yetu itaendelea kuwa kitivo cha kutoa elimu bora kwa kuzingatia misingi yote ya utu wema unaoongozwa na sheria,kanuni, taratibu zilizowekwa na serikali kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia”amesema.

Mtoto Ester Noah Mwanyilu alipotea Mei 18 mwaka huu na Mei 19 taarifa zilitolewa kwa wazazi na walezi na Jeshi la polisi.

Harakati za kumtafuta zilianza kwa shule,wazazi,walezi, Jeshi la polisi,ndugu na marafiki na kuwa Juni 23 mtoto huyo alipatikana akiishi kwenye nyumba moja maeneo ya Ifisi ndani ya halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.