


Na Mwandishi Wetu
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimezindua programu mpya za masomo zinazolenga kuandaa wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika uchumi wa kisasa, huku kikitoa wito kwa Watanzania kutumia fursa za elimu zinazotolewa na chuo hicho ili kuongeza maarifa, kujiendeleza kitaaluma na kujiajiri.
Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa OUT, Dkt. Adam Namamba, amesema chuo hicho kimeendelea kuboresha programu zake ili ziendane na mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia.
Amesema kwa mwaka mpya wa masomo, OUT imeanzisha shahada mbalimbali mpya zikiwemo Sayansi ya Kilimo, Sayansi ya Matumizi na Usimamizi wa Rasilimali Nishati, Usalama wa Mitandao na Uchunguzi wa Kidijitali, Teknolojia za Uchakataji wa Chakula, Usimamizi wa Ukarimu na Matukio, Jiografia na Usimamizi wa Mazingira, Historia na Usimamizi wa Urithi wa Utamaduni, pamoja na Usimamizi wa Safari na Utalii.
“Programu hizi zimeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya uchumi ili wahitimu waweze kujiajiri na kushindana katika soko la ajira,” amesema.
Aidha, amesema chuo kimeanzisha programu maalumu ya Uzamili wa Ualimu wa Elimu ya Msingi, inayowawezesha walimu wenye Stashahada ya Ualimu na uzoefu wa kazi wa angalau miaka miwili kuhitimu ngazi ya uzamili ndani ya miaka mitatu.
Dkt. Namamba amesema OUT ni chuo kikuu cha umma kinachotoa elimu kwa njia huria na masafa, hivyo kuwawezesha wanafunzi kusoma wakiwa popote huku wakiendelea na shughuli zao za kazi, biashara au familia.
Amebainisha kuwa chuo kina vituo 32 nchini na kinahudumia wanafunzi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Pia amesema dirisha la maombi ya uzamili, stashahada za uzamili na uzamivu liko wazi, huku udahili wa cheti, stashahada na shahada kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ukitarajiwa kuanza Julai.
Amewahimiza vijana, wafanyakazi, wafanyabiashara na wakulima kutumia fursa hiyo kujiunga na OUT kwa ajili ya kujenga mustakabali wao kupitia elimu bora na nafuu.

More Stories
Wenyeviti wa Vijiji wamlipua Mbunge kunyang’anywa mihuri
“Serikali inathamini mchango taasisi za dini”
Kihongosi asimulia magumu aliyopitia, ni kilio na furaha