


Na Joyce Kasiki ,Tanga
CHUO Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kimeeleza dhamira yake ya kuendelea kuwa kinara katika ubunifu wa utoaji wa elimu kwa njia ya huria na mtandao kwa kutumia teknolojia na mifumo inayomwezesha mwanafunzi kupata elimu bila kuacha shughuli zake za kila siku.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Chuo, Prof. Alex Makulilo, Kiongozi wa timu ya OUT katika maonesho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Manispaa ya Tanga, kuanzia Agosti 15 hadi 24, 2026, Dkt. Straton Ruhinda, amesema ubunifu ni sehemu muhimu ya mkakati wa Chuo kuhakikisha elimu inawafikia wanafunzi popote walipo.
“Chuo hiki kimekuwa kiongozi katika ubunifu wa zana na mifumo ya kufundishia na kujifunzia, kiasi kwamba mwanafunzi anaweza kusoma akiwa alipo bila kulazimika kufika chuoni mara kwa mara. Wengine wanafika OUT wakati wa mahafali au baada ya kumaliza kabisa. Haya yote yanawezekana kutokana na ubunifu mkubwa uliowekezwa na Chuo,” amesema Dkt. Ruhinda.
Amesema mifumo hiyo imeondoa vikwazo vya umbali na muda, hivyo kumwezesha mwanafunzi kuendelea na masomo sambamba na kazi, biashara na majukumu mengine.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Dkt. Rwejuna, amesema ubunifu katika elimu hauishii kwenye matumizi ya teknolojia, bali unahusisha pia mbinu mpya za ufundishaji, ujifunzaji na utoaji wa huduma.
Amesema OUT inaendelea kutumia TEHAMA, ujifunzaji kupitia mitandao, vifaa vya kidijitali na mifumo ya kisasa ya huduma za wanafunzi ili kuongeza ufanisi, ubora na upatikanaji wa elimu.
“Ubunifu unaiwezesha OUT kuwafikia wanafunzi waliopo katika maeneo mbalimbali nchini na nje ya Tanzania bila kikwazo cha umbali. Teknolojia inamwezesha mwanafunzi kujifunza, kufanya mitihani, kupata huduma za kitaaluma na kuwasiliana na Chuo akiwa alipo,” amesema.
Ameongeza kuwa ubunifu pia unasaidia kuhakikisha programu na mitaala ya Chuo inaendana na mahitaji ya jamii, soko la ajira na mabadiliko ya teknolojia. Kwa OUT, mwanafunzi ndiye kitovu cha huduma, na ubunifu unalenga kuhakikisha kuwa mahali alipo, muda alionao na majukumu yake havizuii fursa ya kupata elimu.
Kupitia ubunifu unaoendelea, OUT inalenga kuimarisha nafasi yake kama kinara wa elimu huria na mtandao nchini Tanzania na taasisi inayovuka mipaka ya kijiografia katika utoaji wa elimu, huku ikichangia kujenga nguvu kazi yenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya karne ya 21.

More Stories
Nmb yaunga mkono afya ya Watumishi kupitia Shimisemita
Ushetu yatoa zabuni za sh.90.48 kwa makundi Maalum
Kahama yatenga sh. bilioni 1.9 kwa zabuni za makundi maalum