April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Othman:Tunahitaji kujipanga zaidi kutatua changamoto za wafanyabiashara

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, amesema Serikali ina wajibu wa kujipanga ili kuhakikisha wanatatua changamoto za kibiashara katika upatikanaji na unafuu wa bidhaa Visiwani Zanzibar.

Othman ameyasema hayo Machi 25, huko soko kuu la Darajani Wilaya ya Mjini Unguja,  baada ya kuhitimisha ziara yake ya kutembelea masoko ili kuona changamoto za wafanyabiashara na upatikanaji wa bidhaa nchini.

Amesema kuwa, kuweka utaratibu bora wa kodi, usafirishaji wa bidhaa na masoko, kutapelekea kupunguza gharama za maisha kwa wananchi hususan katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.

“Serikali kuu itashughulikia hili ila nanyi Mamlaka zinazosimamia biashara hakikisheni hili linakaa sawa ili kuwawezesha wafanyabiashara na wananchi kupata bidhaa kwa urahisi jambo ambalo litasaidi kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wetu”, amesisitiza Othman akielekeza agizo hilo kwa mamlaka zinazohusika ikiwemo Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Ofisi ya Mkuu wa mkoa na Manispaa.

Aidha Othman, amewatakia Wananchi mfungo mwema wa Ramadhan, sambamba na kuwataka waendelee kuiombea dua Nchi hususan katika kipindi hichi ili iendelee kuwa na amani na neema.

Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar,Omar Said Shaaban, amesema Wizara imepokea maagizo na kuhakikisha watayafanyia kazi kwa maslahi ya Wananchi na taifa kwa ujumla.

Akitoa salamu za Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja,Idrisa Kitwana Mustafa, amesema kwakushirikiana na mamlaka nyengine zinazohusika na biashara watajitahidi kuhakikisha miundombinu bora ya biashara inawekwa ili kukidhi mahitaji ya mkoa kibiashara na kupunguza ugumu wa upatikanaji wa bidhaa kwa urahisi na nafuu.

Katika ziara hiyo Othman ametembelea soko la mboga mboga Mombasa, soko la nafaka Kibandamaiti, soko la Samaki Malindi na soko kuu la Darajani yote ya Mjini Magharib Unguja.

Viongozi mbali mbali wameambatana na Mhe. Othman katika ziara hio akiwemo Mstahiki meya wa jiji la Zanzibar Mhe. Mahmoud Mohamed Mussa, Mkuu wa Wilaya ya Magharib B Unguja Bi. Hamida Mussa Khamis na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Ali Khamis Juma