Na Mwandishi wetu , Dar es Salaam
TAASISI ya OpenMap Development Tanzania (OMDTZ) kwa kushirikiana na Serikali imeanza zoezi la kukabidhi Mipango ya Kata ya Kujiandaa na Kukabiliana na Mafuriko kwa jamii katika kata tano za Jiji la Dar es Salaam.
OpenMap inalenga kutumia teknolojia ya ramani, taarifa za kijiografia na ushirikishwaji wa jamii katika kutambua na kupunguza vihatarishi vya majanga.
Zoezi hilo la siku tano kuanzia Septemba 14 hadi 18 ,2026 litaziwezesha kata kupokea mpango na elimu kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kukabiliana na mafuriko endapo yatatokea katika maeneo yao.
Zoezi hilo linalotekelezwa kupitia Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu”, unaofadhiliwa na Zayed Sustainability Prize, linahusisha kata za Keko, Makurumila, Mabibo, Ubungo na Tabata, na linalenga kuwezesha jamii na viongozi kuwa na mipango na taarifa sahihi za maeneo yao kwa ajili ya maandalizi na mwitikio wa mafuriko.
Akifungua rasmi zoezi hilo katika Kata ya Keko, Diwani wa Kata hiyo Ismail Amanzi ameeleza umuhimu wa mipango hiyo kutumika kama nyenzo ya vitendo katika kuimarisha maandalizi ya jamii na kupunguza athari za mafuriko.
“Zoezi hili limekuja wakati sahihi hivyo, ni vyema tukaitumie fursa hii kwa kuhakikisha elimu tunayopewa inafanyiwa kazi kwa vitendo ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa kuzingatia athari za mafuriko katika maeneo yetu,” amesema Amanzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa OpenMap Development Tanzania, Innocent Maholi, amesema ushirikishwaji wa jamii katika kutambua maeneo hatarishi na kuweka taarifa hizo kwenye ramani ni hatua muhimu ya kuhakikisha wananchi wanakuwa sehemu ya kwanza ya maandalizi ya maafa.
“Lengo letu si kutengeneza ramani pekee, bali kuhakikisha taarifa hizo zinatumika na jamii katika kufanya maamuzi na kuchukua hatua kabla ya mafuriko kutokea,” amesema Maholi.
Amefafanua kuwa, kupitia mipango hiyo, wananchi wamewezeshwa kutambua maeneo hatarishi, njia salama za uhamishaji, maeneo ya mikusanyiko na hatua muhimu za kuchukua kabla na wakati wa mafuriko. Zoezi hilo pia linahusisha elimu kwa jamii kuhusu tahadhari za mapema, usafi wa mifereji na hatua za msingi za uokoaji.
Mradi wa “Ramani Zetu, Sauti Zetu” unalenga kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya mafuriko kupitia ramani shirikishi, mipango ya maandalizi ya maafa na matumizi ya taarifa za ndani za jamii katika kuchukua hatua za kupunguza vihatarishi.
Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu yenye dhamana ya kuratibu shughuli za Serikali ikiwemo masuala ya maafa nchini imeendelea kusisitiza umuhimu wa maandalizi ya mapema na ushirikiano kati ya Serikali na jamii katika kupunguza madhara yatokanayo na majanga, hususan wakati wa misimu ya mvua hasa kipindi hiki cha mvua za El Nino.

More Stories
Kairuki: TTCL yafunguka, Tanzania yaingia kwenye Mapinduzi ya Kidijitali
Mradi wa Mawasiliano waongeza ufanisi huduma za Serikali
Kivulini yachochea maendeleo Ilemela