April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyumba ya Wazanaki yanogesha maonesho 77

Na. Mwandishi wetu,Dar es Salaam

NYUMBA ya asili ya kabila la Wazanaki iliyojengwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Taasisi yake ya Makumbusho ya Taifa, imekuwa kivutio kikubwa kwenye Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam Maarufu kama Saba Saba.

Makundi Makubwa ya watanzania , wanaofika katika Maonesho hayo ya Kimataifa licha ya kupata huduma zingine kwenye banda la Maliasili na Utalii, wametembelea Nyumba hiyo na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu Kabila la Wazanaki lenye historia kubwa kupitia Rais wa kwanza wa Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere.

Akizungumza leo katika maonesho hayo,Mhifadhi Mila Mwandamizi wa Makumbusho ya Taifa, Flora Vincent amesema kuwa sababu ya kuwa na onesho la Nyumba ya asili kwenye maonesho hayo makubwa ni kuipa fursa jamii kujifunza umuhimu wa kurithisha kizazi kilichopo Mila na Desturi za Makabila mbalimbali ili kuimarisha Mshikamano wa Kitaifa, Umoja, Upendo, amani Kwa maendeleo endelevu nchini.

Akizungumzia maonesho hayo, Debora Danishashe amesema ameamua kuwaleta wajukuu zake kwenye nyumba hiyo ili wapate uwelewa juu ya Urithi wa Utamaduni, wa makabila mbalimbali ya Tanzania.

Danishashe ameongeza kuwa, kizazi cha sasa kimetawaliwa na ulimwengu wa utandawazi unawafanya waige tamaduni za nje na kusahau zao hivyo ubunifu uliofanywa na Wizara ya Maliasili ya kuwarithisha watu hasa watoto Utamaduni wa Kitanzania ni jambo jema la lakupongezwa sana.

Katika Banda la Maliasili na Utalii, wananchi wanapata fursa mbalimbali za kufahamu huduma zinazotolewa na Wizara hiyo, Taasisi na Idara zake kama sehemu ya kuwasigezea karibu huduma zinazohitajiwa na Jamii katika sekta ya Malisili, Wanyamapori, Malikale, Misitu, Nyuki, Utalii na Elimu.