April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo

Nyongo apiga marufuku vishoka kwenye Soko la Madini Tunduru.

Na, Pius Nkanabo, Tunduru

NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amepiga marufuku  watu wanaofanya biashara nje ya mfumo wa masoko yaliyoanzishwa maarufu kama vishoka na kuongeza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Nyongo ameyasema hayo jana kwenye mkutano wake na wafanyabiashara wa madini katika Soko la Madini Tunduru ikiwa ni sehemu ya ziara yake kwenye soko hilo yenye lengo la kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye uendeshaji wa soko hilo.

Katika kikao hicho  Nyongo ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Ruvuma, Isaack Ngerangera, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Getty Massawe, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephraim Mushi na  Afisa Utawala wa Tume ya Madini, Saashisha Mafuwe.

Amesema kuwa, katika Soko la Madini la Tunduru wapo watu wasio waaminifu wamekuwa wakifanya biashara ya madini nje ya soko la madini lililoanzishwa na kuongeza kuwa Serikali haitawafumbia macho kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi kutokana na kukwepa kodi mbalimbali zinazotakiwa kulipwa Serikalini.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inakuja na mkakati mpya wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa madini wanatumia masoko ya madini yaliyoanzishwa.

Katika hatua nyingine Nyongo amesema kuwa ili kuhakikisha wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na shughuli za uchimbaji wa madini, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli iliamua kufuta kodi nyingi zilizokuwa kero  kwa wachimbaji wa madini pamoja na uanzishwaji wa masoko ya madini.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo

Katika hatua nyingine, Nyongo amewataka maafisa madini wakazi nchini kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama na Taasisi nyingine za Serikali.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Nyongo amemsimamisha kazi aliyekuwa Mkaguzi Msaidizi wa Madini, Athumani Masawe ambaye ametuhumiwa na wanunuzi wa madini kuhusika na kufanya biashara nje ya soko kinyume na sheria ya madini.

Aidha amekemea vikali tabia ya viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Wilaya ya Tunduru kuingilia shughuli za uuzaji na ununuzi wa madini ndani ya Soko la Madini la Tunduru.

Katika hatua nyingine amempongeza Mkuu  wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwenye sekta ya madini ikiwa ni pamoja na kuwasimamisha viongozi wa Chama cha Wachimbaji wa Madini  Wilaya ya Tunduru kwa kuingilia shughuli za uendeshaji wa Soko la Madini la Tunduru.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amempongeza Naibu Waziri Nyongo kwa kufanya ziara kwenye soko hilo na kutatua changamoto zilizojitokeza na kuongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa  Mkoa wa Ruvuma kwenye usimamizi wa Soko la Madini Tunduru ili liwe na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini.