April 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NMB yazindua kifurushi maalum kwaajili ya walimu

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa Rai kwa benki ya NMB kuhakikisha inawafikia watumishi wengi zaidi wakiwemo walimu ili kuwasaidia kujiendeleza kimaisha.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akizungumza na walimu wa Shule za Msingi na Sekondari wa kanda ya Kati Jijini  Dodoma katika siku ya Mwalimu iliyoandaliwa na benki ya NMB ikienda sambasamba na uzinduzi wa Mpango wao  Maalum wa “Mwalimu Spesho.” 

Mpango huo ni kwa ajili ya walimu kupata mikopo na huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo nchini huku walimu wakipongeza huduma hizo.

Waziri alisema mpango huo mzuri usiishie kwa walimu 5,000 badala yake angetamani uwafikie walimu wengi na watumishi ili kuwajengea uwezo hasa walimu ambao ndiyo chanzo cha kuwaandaa viongozi, wataalamu wa baadae.

Alitaka NMB kusimama na walimu wakati wote ili kuwajengea uwezo akieleza kuwa jumla ya walimu 6800 wamepandishwa madaraja hivyo ni fursa kwao kuingia kwenye mikopo kwa benki ambayo inajulikana na uendeshaji wake mzuri kuliko kukopa kwenye taasisi ambazo zinawaumiza.

Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi alisema walikusanya walimu viongozi 350 kwa ajili ya kubadilishana mawazo kuboresha zaidi huduma za kibenki na kujadiliana kuhusu fursa zilizopo kwa ajili ya kundi la Walimu nchini.

“Tunaamini, walimu hawa zaidi ya 350, watasaidia kupeleka elimu watakayoipata hapa kwa wenzao na hata familia zao na jamii kwa ujumla juu ya huduma nzuri zinazotolewa na benki ya NMB, lengo ni kumfanya mwalimu kuwa na maisha mazuri wakati wote,” alisema Mponzi.

Hoja ya NMB ilianzia kwa mbunge wa Viti Maalumu, Dkt. Teya Ntala ambaye aliomba mabenki mengine kuiga mfano wa benki hiyo kwani imekuwa ni sehemu ya kuigwa mfano kwa wanyonge.

Aidha, Benki ya NMB inatoa mikopo mingi ikiwemo bima ya kujikinga na majanga mbalimbali, mikopo ya elimu kwa walimu na wategemezi wake, mikopo ya kilimo,uvuvi na ufugaji, mikopo ya vyombo vya moto vya binafsi na biashara na mikopo ya wakulima wadogo wadogo.  

Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi (kushoto)  akishirikiana na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama kutoa kitambaa ikiwa ni ishara ya kuzindua Mpango maalum wa ‘Mwalimu Spesho’ iliyozinduliwa jana Jijini Dodoma.
Afisa Mkuu Wateja Binafsi na Biashara Benki ya NMB, Filbert Mponzi (watatu kushoto) akimpa maelezo Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama mara baada ya kuzindua Mpango maalum  ‘Mwalimu Spesho’ uliyozinduliwa jana Jijini Dodoma. Wapili kushoto ni Mkuu wa Idara ya wateja Binafsi, Aikansia Muro na Meneja kanda ya Kati Nsolo Mlozi.