May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NIT yaiomba China kuharakisha mchakato ujenzi Chuo Kikuu cha Usafirishaji

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Chato

CHUO cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) kimeiomba Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kuharakisha mchakato wa kuanza ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Usafirishaji baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu.

Mpango huo wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Usafirishaji unahusisha pia vyuo vikuu vitano vya usafirishaji barani Afrika ambavyo vimo katika mkakati wa Serikali ya China wa kujenga au kuendeleza vyuo vya usafirishaji kwa hadhi ya chuo kikuu.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari hivi karibuni wilayani Chato katika ziara ya Waziri wa Mambo ya nje wa China, Wang Yi alipotembelea Tanzania, Mkuu wa Chuo cha NIT Profesa Zacharia Mganilwa amesema;

“Nimekuja kwenye ziara hii kuiomba Serikali ya China kupitia kwa Waziri Wang Yi mchakato huu wa ujenzi wa kukibadilisha chuo chetu kuwa Chuo Kikuu uweze kwenda kasi kidogo, hivi sasa tumeshakamilisha upembuzi yakinifu ambapo chuo chetu kitakuwa kati ya moja ya vyuo vikubwa barani Afrika.”

Profesa Mganilwa ameongezea; “Ujenzi wa chuo hiki utagharimu zaidi ya sh. Bilioni 130 na kitakuwa chuo bora kabisa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.”

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa akiwa na Makamu wa Rais wa Chuo Kikuu cha Dalian Maritime Prof. Shan Hongjun mara baada ya Prof Mganilwa kutembelea nchini China mwaka 2015.

Amesema kuwa kukamilika kwa Chuo Kikuu cha Usafirishaji utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza rasilimali watu katika miradi mikubwa ya usafirishaji ambayo inaasisiwa na serikali ya awamu ya tano ikiwamo ujenzi wa reli ya treni ya mwendo kasi (SGR), Shirika la ndege la Tanzania ATCL pamoja na miradi ya ujenzi wa meli pamoja na barabara.

“Upembuzi yakinifu uliofanywa na Chuo Kikuu cha Southwest Jiaotong cha nchini China ulimalizika tangu mwaka juzi 2018, tunatarajia kuona mradi wa ujenzi ukianza,” amesema.

Mbali na kuwa na ndaki tano, Chuo Kikuu kitakuwa na ofisi, maabara, vyumba vya mikutano maktaba na hosteli za wanafunzi.

“Kutokana na China kuwa na teknolojia za kisasa kabisa, tunatarajia kupokea mashine za kufundishia za teknolojioa ya juu hasa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa chuo,”amesema.

Prof Mganilwa amesema kuwa kupandishwa hadhi kwa NIT kuwa Chuo Kikuu ni muhimu sana kwa Watanzania kwa sababu nchi inahitaji wataalam zaidi wa uchukuzi na usafirishaji katika kukuza uchumi wa nchi.

Amesema kuwa kuwepo kwa chuo Kikuu hicho kutaweza pia kuzisaidia nchi jirani kama Kenya, Uganda, Kongo DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, Malawi na Zambia ili na wao waweze kupata mafunzo.

Amesisitiza: “Afrika Mashariki na Kati hakuna Chuo Kikuu cha uchukuzi na usafirishaji, hivyo chuo hiki kitakapo kamilika kitaweza kuwasaidia Watanzania na majirani zetu.”

Pamoja na hayo, Balozi wa China nchini, Wang Ke alimweleza Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ilipomtembelea Ikulu Jijini Dar es Salaam kwamba China imeridhia kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo.

Balozi Wang alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya misaada na miradi mbalimbali ambayo China inaitekeleza nchini Tanzania yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na Tanzania.

Mwakilishi wa Serikali ya China wa masuala ya uchumi na biashara, Lin Zhiyong amewahi kutembelea eneo la mradi huo ambalo ni chuo cha NIT kilichopo Mabibo, jijini Dar es Salaam.

Amesema ujenzi wa majengo mapya katika chuo hicho unatarajia kuanza muda si mrefu na ni utekelezaji wa ahadi ya Rais wa China, Xi Jinping, aliyoitoa akiwa Afrika Kusini mwaka 2015.

Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Profesa Zacharia Mganilwa, akizungumza na waandishi wa habari.

Pamoja na hayo, idadi ya wanafunzi katika Chuo cha Taifa Cha Usafirishaji imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, hivyo kuongeza idadi wa taalamu katika sekta ya uchukuzi na usafirishaji.

“Idadi ya wanafunzi imeongezeka kwa miaka 7 kwa asilimia 258 kutoka wanafunzi 3248 kwa mwaka wa masomo 2014/15 mpaka wanafunzi 11640 mwaka 2019/20.

“Kwa sasa chuo kinawafanyakazi 327 ikiwa wanataaluma ni206 na waendeshaji 121. Idadi hii ya wanataaluma ni ndogo kulinganisha na uhitaji wake na hivyo chuo kimekuwa kikitumia fedha nyingi kulipa walimu wa muda. Hivyo tunaamini kwa mwaka huu wa fedha tunaweza kupata kibali cha kuajiri na hivyo kutatua tatizo hili,” amemalizia Mkuu wa Chuo cha NIT.