May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa kilimo cha mpunga JKT kuzalisha chakula cha kutosha

Na Joyce Kasiki, TimesMajira,Online,Chita

JESHI la Kujenga la Taifa (JKT) linatarajia kuzalisha chakula cha kutosha kupitia mradi wake wa kilimo cha mpunga unaotekelezwa katika kikosi cha 837 KJ, Chita JKT mkoani Morogoro.

Jeshi hilo linatarajia kulima zao hilo mara mbili kwa mwaka kupitia skimu ya umwagiliaji ambayo hivi sasa kazi ya kujenga mifumo ya skimu hiyo inaendelea.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mifumo ya skimu hiyo, Mkuu wa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge alisema,mradi huo unatarajia kukamilika Mei, mwaka huu kwa gharama sh. bilioni nne.

Hata hivyo, Meja Jenerali Mbuge ametoa wito kwa Serikali kuliunga mkono jeshi hilo kwa kusaidia fedha ili liweze kupanua miundombinu inayojengwa katika eneo hilo kwa lengo la kuongeza uzalishaji zaidi.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni mtaji ,sisi tumeamua kutekeleza mradi huu kwa kutumia fedha zetu za ndani kiasi cha sh. Bilioni 4 katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji.

“Wito wangu kwa Serikali itusaidie fedha ili tuweze kupanua miundombinu hii ili tuweze kulima ekari 12,500.”Amesema Meja Jenerali Mbuge.

Umwagiliaji dawa shamba na mpunga

Aidha Mkuu huyo wa JKT alisema mradi huo ni mzuri kwani utawawezesha kulima mara mbili kwa mwaka, lakini pia utawawezesha kufuga samaki kutokana na wingi wa maji yaliyopo katika eneo hilo na hivyo kuliwezesha Jeshi hilo kuuza na kupata fedha zitakazosaidia kulisha vikosi vingine.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Hassan Mabena amesema kazi iliyofanyika katika skimu hiyo katika awamu ya kwanza ya ujenzi ni kuhakikisha maji yanayotiririka kutoka katika mito inayopita katika kikosi cha Chita ,yanapita katika mifumo inayojengwa na katika mitaro mama na baadaye yatakwenda na kupita katika vigawa maji na kuelekezwa mashambani.

“Lakini awamu ya pili itakuwa ni kutengeneza mitaro mikubwa na midogo ambayo kazi yake ni kuingiza maji na kutoa maji mashambani,” amesema Kanali Mabena na kuongeza;

“Kwa mujibu wa wataalam wetu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakishirikiana na wataalam wa ndani ya JKT ,kazi hiyo itafanyika hadi kufikia mwezi Mei na Juni vitatengenezwa vijaruba ili maji yaweze kuingia na kutoka mashambani.”

Aidha amesema katika utafiti uliofanyika awali eneo liloonekana linafaa kwa kilimo ni ekari 12,500 lakini kutokana uwezo wetu tutaanza na kulima ekari 2,500.

Naye Mtaalam kutoka Tume ya Umwagiliaji ambaye ndiye msimamizi wa mradi huo Mhandisi Elbariki Mwendo, alisema wazo la mradi huo ni zuri kwani litaiwezesha nchi kujitosheleza kwa chakula kupitia JKT.