June 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Namibia yaenzi historia ya ukombozi Kongwa

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Kongwa 

RAIS wa Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah,ameipongeza  Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika harakati za ukombozi wa Namibia na nchi nyingine za Kusini mwa Afrika.

 Dkt.Nandi- Ndaitwah amezungumza hayo leo Juni 21,2026 Wilayani Kongwa Jijini  Dodoma,katika  ziara yake ya kikazi Tanzania ambapo ametembelea kambi ya wapigania uhuru wa Namibia iliyopo wilayani Kongwa na kukagua eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Namibia katika Mji wa Serikali Mtumba.

Katika  ziara hiyo, Dkt. Nandi-Ndaitwah alifika katika eneo la makaburi ya mashujaa wa Namibia waliopigania uhuru wa taifa lao na kuweka mashada ya maua katika Makaburi matatu  kama ishara ya heshima na kumbukumbu kwa wapigania uhuru hao. 

Aidha, alipata fursa ya kutembelea makazi pamoja na hospitali iliyokuwa ikitumika kutoa huduma za matibabu kwa wapigania uhuru hao walipokuwa wakipata mafunzo na hifadhi nchini Tanzania.

Rais huyo pia alikutana na familia zenye asili ya Namibia zinazoishi Kongwa na kusalimiana nazo kabla ya kuzungumza na wananchi pamoja na wageni mbalimbali waliojitokeza katika eneo la makaburi ya mashujaa hao.

Dkt.Nandi-Ndaitwah ameeleza kuwa Kongwa ilikuwa moja ya maeneo muhimu yaliyotumika kuwapa mafunzo na kuwahifadhi wapigania uhuru wa nchi hiyo wakati wa mapambano dhidi ya ukoloni.

“Nashukuru sana. Tulipigania uhuru pamoja na nyie na leo tupo hapa Kongwa. Mahali hapa palikuwa sehemu muhimu ya ukombozi kwa nchi za Kusini mwa Afrika. 

“Hata mume wangu alikuwa katika kundi la pili la waliokuja hapa na alipata mafunzo yake ya kijeshi Kongwa. Kwa sisi wananchi wa Namibia, eneo hili ni kama nyumbani kwetu,”amesema Rais Nandi-Ndaitwah.

Ameeleza kuwa historia ya ushirikiano kati ya Tanzania na Namibia inapaswa kuhifadhiwa na kuenziwa ili vizazi vijavyo viweze kujifunza mchango wa viongozi na wananchi waliopigania uhuru wa mataifa yao.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha mahusiano yaliyopo kati ya nchi hizo mbili kwa kushirikiana katika sekta mbalimbali za maendeleo. 

Ametaja  maeneo ya biashara, uwekezaji, elimu na maendeleo ya kijamii kuwa miongoni mwa nyanja zinazoweza kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa Tanzania na Namibia.

Ziara  hiyo imeendelea kudhihirisha uhusiano wa kihistoria na kidugu uliopo kati ya Tanzania na Namibia, huku ikitoa fursa ya kuenzi mchango wa wapigania uhuru na kuimarisha ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo mawili.