May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Ridhiwani awaonya wenyeviti wa mabaraza ya Ardhi nchini

Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tanga

Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amewaonya wenyeviti wa mabaraza ya ardhi nchini kujiepusha na tabia ya rushwa ambayo tayari imeshaanza kuota mizizi nchini huku akisema uzembe na ubabaishaji kwa wateja wao hauna nafasi katika Tanzania ya leo inaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua mkutano wa wenyeviti wa mabaraza ya ardhi ya wilaya nchi nzima unaofanyika jijini Tanga kwa siku 4.

Naibu Waziri huyo wa ardhi amewataka wenyeviti wa mabaraza hayo ya ardhi nchini kujiepusha na vitendo vinavyoharibu mifumo ya upatikanaji wa haki kwa wananchi ikiwemo suala la rushwa.

“Jiepusheni na vitendo vya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki wananchi wetu wamekata tamaa na mabaraza haya hivyo kuna haja yakuja na mabadiliko yatakayosaidia kuongeza imani, “amesisitiza Ridhiwani.

Aidha Naibu waziri Ridhiwani amewataka wenyeviti hao kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa mabaraza hayo na mabadiliko mbalimbali ya sheria yanayotokea ambayo ni muhimu kwa wananchi kuyafahamu.

Sambamba na hayo amewataka watumishi wa sekta ya ardhi nchini kuwa kila mmoja atimize wajibu wake kwa kutoa huduma bora kwani mamlaka za nidhamu zinasisitiza kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wasiotimiza wajibu wao na wanaoidhalilisha serikali kwa kutenda vitendo visivyofaa ikiwemo kupokea rushwa.

Kwa upande wake Katibu mkuu wa wizara ya ardhi nyumba na maendeleo ya makazi Dkt. Allan Kijazi katika kikao hicho amewataka watendaji hao kuwa tayari kubadilisha taswira ya wizara ya kiutendaji kutoka wizara ya malalamiko na badala yake iwe wizara ya kupewa sifa nzuri kiutendaji.

“Kitanzi chetu kipo hapa hapa Tanga mdio hukumu ya utendaji wenu utakapoanzia na wale ambao utendaji wao utaridhisha basi tutakuwa pamoja nao na wale ambao hawatotaka kubadilika watupishe tutafute watendajiau wenyeviti ambao wapo tayari kutekeleza majukumu yao na wapo tayari kutenda haki kwa watanzania wote bila kubagua, “amesisitiza katibu mkuu Dkt Kijazi.

Lengo kubwa la kikao hicho ni kuwakumbusha wenyeviti wajibu wa kutekeleza majukumu kwa mujibu wa kanuni zinavyowaongoza hivyo kikao hicho kitawakumbusha wajibu na kanuni zilizopo na kwamba migogoro yote inayowasilishwa kwenye mabaraza ikamilike ndani ya miaka miwili.