May 13, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri Kigahe ataka uadilifu mpaka wa Tunduma

Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Tunduma.

NAIBU Waziri Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amewataka watendaji katika kituo cha pamoja cha forodha {OSBP} katika mpaka wa Tunduma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Kigahe ametoa rai hiyo Agosti 9, 2023 mara baada ya kutembelea taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo katika kituo hicho cha pamoja cha forodha {OSBP}katika mpaka huo wa Tunduma, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili mkoani Songwe.

Amesema kuwa, kama Watendaji wa Wizara hiyo na wale wa taasisi nyingine za serikali katika mpaka huo wakitekeleza majukumu yao kwa uadilifu watajenga imani kubwa na kuifanya Tanzania kuwa chaguo namba moja kwa mataifa yanayotumia bandari ya Dar-es-Salaam kupitisha mizigo yao.

“Nilipotembelea na kujionea utendaji kazi kwenye taasisi zilizopo chini ya Wizara yetu katika mpaka huu nimesisitiza watendaji kuacha ukiritimba , ikiwemo kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha ili kurahisisha ufanyaji biashara kwa wafanyabiashara wa ndani au kutoka nje ya nchi,”amesisitiza Kigahe.

Kigahe ambaye katika ziara hiyo ameongozana na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Biashara Dk. Anifa Mohamed , pamoja na Mkurugenzi wa wakala wa vipimo nchini (WMA) Silaji Moyo, amesema Tanzania kupitia mpaka wa Tunduma inahudumia mataifa sita ya Zambia, Zimbabwe, Afrika Kusini, Namibia, Botswana na Kongo.

Aidha, Naibu Waziri Kigahe amekemea tabia ya urasimu kwa watendaji kwani kufanya hivyo kutazorotesha adhma na juhudi za serikali katika kutekeleza mpango wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kigahe ametoa maelekezo kwa Wakala wa Vipimo nchini {WMA} kuhakikisha wanafanya ukaguzi ili kujiridhisha kama bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia mpaka huo vipo kwenye vipimo halisi ili watumiaji wasipunjwe.

Mbali na kupima pia ametaka wakala hao kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuwajengea uwezo na kuona umuhimu wa kutumia bidhaa zilizo kwenye vipimo halisi, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutumia vipimo visivyo na uhalisia kama BP na Lumbesa.

Wakati huo huo amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa nchini kupitia mpaka huo wa Tunduma zinakaguliwa ili kulinda afya za watumiaji.

Awali akitoa taarifa ya Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Songwe,Dk. Francis Michael amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa, licha ya mkoa huo kuwa kinara wa uzalishaji wa mazao ya kilimo kama mpunga na mahindi lakini bado hawanufaiki kutokana na kuuza mazao yao kwa kutumia vipimo batili.

Hivyo, aliomba kuimarishwa kwa wakala huo ili kuwa na nguvu ya pamoja ili kusimamia matumizi ya vipimo.