May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

NACOPHA yaeleza mambo yanayochangia jamii kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Kwa mujibu wa utafiti Tanzania HIV Indicators Survey(THIS)kwa mwaka 2016-2017,kiwango cha maambukizi ya Ukimwi kitaifa Tanzania Bara ni asilimia 4.7 na kwa Mkoa wa Mwanza ni asilimia 7.2.

Ambapo imeelezwa kuwa hadi sasa tafiti nyingi zilizofanyika sehemu mbalimbali nchini zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi wanaulewa Ukimwi unavyoambukizwa na njia za uambukizaji.

Hata hivyo jamii imekuwa katika hatari ya kuambikizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU),kutokana na mambo mengi yanayochangia kama vile mila hasi za kurithi na kutakasa wajane.

Akisoma risala Katibu wa Baraza la Taifa la watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi(NACOPHA) Wilaya ya Nyamagana Joseph Kiharata katika maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo uadhimishwa Kila ifikapo Desemba 1,kila mwaka ambapo kimkoa yamefanyika uwanja wa Mirongo wilayani Nyamagana ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo,”Imarisha Usawa”.

Kiharata ameeleza jamii imekuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya VVU kutokana na kuendelea kuwepo kwa tabia na baadhi ya mila na desturi mbaya zinazojenga mazingira hatarishi ya maambukizi.

Huku watoto wengi hasa wa sekondari ambao wengi wao wapo kwenye umri balehe na kuanza kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi.

“Tabia hatarishi zilizopo mkoani Mwanza kama vile ulevi wa kupindukia,ngono zembe, wapenzi wengi,ndoa na mimba za utotoni,ngono katika umri mdogo,ngoma za mapacha,kutumia nyembe zisizo salama,matumizi ya dawa za kulevya, mapenzi ya jinsia moja,biashara ya ngono poja na umaskini pia ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuchangia jamii kuwa katika hatari ya kupata maambukizi VVU,”ameeleza Kiharata.

Mbali na hilo pia ameeleza kuwa mashirika mengi yanayojushughulusha na masuala y Ukimwi bado hayajaweza kufika vijijini ambako ndipo kwenye changamoto hasa mtu akipimwa na kugundulika kuwa ana VVU.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda NACOPHA Mwanza Veronica Joseph, ameeleza kuwa wanatelekeza mradi wa ebu tuyajenge chini ya ufadhili wa USAIDS,kwa lengo la kufikia 95 tatu.

Ambapo 95 ya kwanza ni kuhamasisha watu wakapime na kujua afya zao,95 ya pili watu wakiisha jua afya zao na watakaogundulika kuwa na maambukizi ya VVU waanze kutumia dawa za kufubaza virusi (ARVs) na watawafuatilia kuhakikisha wanatumia dawa hizo.

Huku 95 ya tatu ni baada ya kuanza kutumia dawa wapime wingi wa virusi kuona zile dawa wanazozitumia kama zinawasaidia vizuri kufubaza VVU.

“Mradi huu tunautekeleza kwa kuwatumia mawakili tiba ambao ni mtu aliefaulu vizuri kutumia dawa ambaye ataweza kumuhamisha mwenzie kutumia dawa,ambao umewafikia vijana na watu wazima,”ameeleza Veronica.

Mbali na hayo ameeleza kuwa wana programu za kutoa elimu shuleni na vyuoni ili waweze kupima na wakikutwa na maambukizi waanze kutumia dawa vizuri.

Naye Mkurugenzi wa shirika la Kivulini Yassin Ali, ameeleza kuwa kuna mahusiano ya karibu kati ya ukatili wa kijinsia na maambukizi ya VVU,hivyo jitihada zao zitahitaji kuelekezwa kushughulikia mahusiano hayo yaliopo.

“Ukuchukua takwimu za hivi karibuni za we zetu Jeshi la Polisi za Januari hadi Septemba mwaka huu,inaonesha matukio yanayoongoza ya ukatili wa kijinsia kwa watoto wenye umri wa miaka 0-17, ubakaji ni 4757,kuwapa wanafunzi mimba 1115, ulawiti 1044 ambapo wakiume ni 778 na wakike ni 166,”

Yassin ameeleza kuwa wabakaji,wanaowapa wanafunzi mimba na kufanya vitendo vya ulawiti vinaweza kuathiri mtoto pia kupata maambukizi ya VVU hivyo alitoa wito kwa wote wanaofanya vitendo hivyo mkono wa sheria ufanye kazi dhidi yao.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima, akizungumza katika maadhimisho hayo,alitoa rai kwa wadau, viongozi na jamii kutafakari mambo gani yanayochangia kiwango cha maambukizi ya VVU mkoani humo na wachukue hatua ili kudhibiti ongezeko la maambukizo hayo kwani bado yako juu ukilinganisha na kiwango cha kitaifa.

Ameipongeza NACOPHA kwa jitihada za kuelimisha na kufuatilia makundi mbalimbali ya wanaoishi na VVU huku akiwataka wananchi wanaopata elimu juu ya VVU wakaifanyie kazi.

Katibu wa NACOPHA Konga ya Wilaya ya Nyamagana Joseph Kiharata akisoma risala wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani ambayo uadhimishwa Kila ifikapo Desemba mosi ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kimkoa kwa Mkoa Mwanza yamefanyika katika uwanja wa Mirongo wilayani Nyamagana jijini Mwanza.
Meneja wa Kanda NACOPHA Mwanza Veronica Joseph, akizungumza na TimesMajira Online mara baada ya kumalizika kwa maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani ambayo uadhimishwa kila ifikapo Desemba mosi kila mwaka.