July 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wazindua jengo lenye thamani ya bil 3.4

*Kiongozi Mbio za Mwenge ampongeza Mkurugenzi,asisitiza miundombinu kulindwa

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mbulu

MWENGE wa Uhuru 2026 umezindua rasmi jengo jipya la utawala la Halmashauri ya Mji wa Mbulu mkoani Manyara,lenye thamani ya zaidi ya sh.bil 3.4,hali inayolenga kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi ,ujenzi ulianza Agosti 2023 na kukamilika Juni 30, 2026.

Akizungumza leo mara baada ya kuzindua jengo hilo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya utawala unalenga kuongeza ufanisi wa utendaji wa watumishi na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.

Huku akimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu Rehema Bwasi kwa usimamizi mzuri na makini wa ujenzi huo.

“Miradi kama hii inaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha utawala na kuboresha huduma kwa wananchi.Ni wajibu wetu kuhakikisha miundombinu hii inalindwa na kutumika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,”amesema Mwang’onda.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kudumisha amani,umoja na mshikamano ili kuweka mazingira bora ya maendeleo na kuhakikisha uwekezaji wa Serikali unaendelea kuwanufaisha wananchi.

Hata hivyo katika utekekalezaji wa mradi huo zaidi ya sh.bil 2.52 zimetumika kwenye ujenzi huku sh.mil 300 zikitumika kwenye ununuzi wa samani.Ambapo jengo hilo ni la ghorofa moja ambalo Lina vyumba 62 na kumbi mbili za mikutano.

Aidha mradi huo umetekelezwa kwa utaratibu wa ‘Force Account” chini ya fundi Mjenzi SUMA JKT na tayari umeanza kutumika, ukitarajiwa kuimarisha uratibu wa shughuli za halmashauri na kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kiutawala kwa wananchi.