August 29, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWADETA yawanoa walimu mahitaji maalumu

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online-Mwanza

TAASISI ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA) imetoa mafunzo kwa walimu wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalumu katika shule za awali na msingi Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.

Huku lengo la mafunzo  hayo ni kuwaongezea uelewa walimu hao, kuhusu elimu jumuishi na namna ya kuwahudumia watoto wenye changamoto mbalimbali ikiwemo wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Mafunzo hayo yamefanyika Agisti 28,2026 katika Shule ya Msingi Buswelu iliopo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ambapo Mkurugenzi wa MWADETA Walter Miya  amesema, taasisi hiyo inalenga kuendelea kutoa elimu kuhusu ujumuishi wa watoto wenye mahitaji maalumu shuleni.

Miya amesema,awali MWADETA ilianza kutoa elimu hiyo katika Wilaya ya Nyamagana na sasa imehamia Ilemela ili walimu wapate uelewa wa namna ya kuwahudumia watoto wenye mahitaji maalumu wanapokuwa shuleni.

Amesema,changamoto iliokuwepo ni baadhi ya walimu kutokuwa na uelewa wa namna ya kuainisha watoto wenye changamoto hizo, lakini kupitia mafunzo hayo wameanza kuwabaini na kuelewa mahitaji yao wakiwa katika madarasa yao.

Pia amesisitiza umuhimu wa watoto hao kufundishwa ujuzi mbalimbali wa kujitegemea ikiwemo kujisafisha,ili waweze kushiriki katika shughuli za kila siku kwa kujiamini.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu Maalumu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Mwalimu Zakia Rashid amesema,mafunzo hayo yamewaongezea walimu ujuzi na maarifa ya kuwahudumia watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa.

Mwl.Rashid amesema,changamoto kubwa ilikuwa namna ya kuwahudumia watoto hao, hasa wenye mgongo wazi, ambao wanaweza kujisaidia haja ndogo na kubwa bila kujua,Hivyo kupitia mafunzo hayo ya nadharia na vitendo yamewasaidia kujua namna ya kuwapatia huduma stahiki na kuwafanya wawe wasafi na nadhifu wakiwa shuleni.

Hata hivyo amesema,watoto wenye mgongo wazi katika hatua za awali hutengwa katika madarasa ya vitengo yenye idadi ndogo ya wanafunzi ili waweze kupata huduma inayostahili, huku kiwango cha ulemavu wa kila mtoto kikizingatiwa katika upangaji wa wanafunzi.

Mwalimu wa Elimu Maalumu wa Shule ya Msingi Kirumba, Michael Mwilenga amesema,watoto wenye mahitaji maalumu mara nyingi huhitaji ufundishaji wa kurudia rudia, tofauti na mpangilio wa kawaida wa somo, hivyo ni muhimu kuwa na madarasa na walimu wenye utaalamu kulingana na mahitaji yao.

Amesema,changamoto nyingine ni ushirikiano mdogo kutoka kwa baadhi ya wazazi wenye watoto wenye mahitaji maalumu, ambao hupeleka watoto shuleni lakini hawafuatilii maendeleo yao, hivyo akawataka wazazi kushirikiana na walimu katika malezi na elimu ya watoto hao.

Mama wa mtoto mwenye changamoto ya mgongo wazi, Teddy Phineas amesema,kabla ya kupata elimu ya namna ya kumhudumia mtoto wake ikiwemo kumsaidia kutoa haja kubwa na ndogo, alikuwa akikumbana na unyanyapaa.

Hivyo ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya shule kwa kuhakikisha vyoo vinakuwa karibu na madarasa ili watoto hao waweze kupata huduma kwa urahisi,ili wazazi wasilazimike kuacha shughuli zao za kiuchumi mara kwa mara kuwafuata watoto shuleni.