May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mutta Rwakatale ahimiza maadili mema kwa watoto

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online,Dar

MKURUGENZI wa shule za St. Mary’s Mutta Rwakatale ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwasimamia watoto na kuhakikisha kuwa wanakuwa katika maadili mema sambamba na kuwanapatia elimu ikiwa ni haki yao kwa mujibu wa sheria.

Alitoa wito huo mwishoni mwa wiki katika mahafali ya kuwaaga wanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo yaliyofanyika kwenye shule ya St Mary’s Mbagala mkoani Dar es Salaam, ambapo alisema kumpatia elimu mtoto kunamsaidia asiwe tegemezi baadaye.

Alisema kila mzazi anajukumu la kuhakikisha kuwa anamwelimimisha mwanaye kwa hali yoyote ile ili atakapokuwa aweze kumsaidia na kusisitiza kuwa watoto wanahaki ya kusikilizwa katika mahitaji yanayowasaidia kutimiza malengo yao.

Mkurugenzi wa shule za St Mary’s Mutta Rwakatale akimkabidhi cheti mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo wanaomaliza darasa la saba kwenye mahafali yaliyofanyika shuleni hapo. Kulia ni Mkuu wa shule hiyo, Jacob Mwangi

“Mtoto anapokuomba umpeleke kwenye masomo ya ziara wakati wa likizo, umnunulie daftari, kalamu na vitu vingine vinavyomsaidia katika masomo yake jitahidi umpatie kwani mafanikio yake ni furaha kwetu sisi walimu kwenu wazazi na kwake pia, watoto ndio viongozi, madaktari, marubani walinzi na nguvukazi ya taifa kwa baadae tuwalinde na kuwarithisha elimu bora.

“Tuwe na tabia ya kuwajenga watoto watu kiimani tukifanya hivyo watakuwa na hofu, wengine ni wakorofi lakini tukiwa na kawaida ya kuongea nao kwa kuwaelekeza taratibu watakuelewa,” alisisitiza.

Aliwataka wazazi pia kuwasisitiza wanafunzi hasa wa darasa la saba wanaotarajia kufanya mtihani wa kuhitimu wiki mbili zijazo kuhakikisha kwamba wanasoma kwa bidii ili watimize malengo yao.

Mkurugenzi wa shule za St Mary’s Mutta Rwakatale akifurahia jambo na wahitimu wa darasa la saba wa shule hiyo upande wa Mbagala wakati wa mahafali yaliyofanyika shuleni hapo mwishoni mwa wiki

Aidha, watoto wanategemewa na familia na taifa kwa ujumla hivyo wanapaswa kujilinda na kuwa na tahadhari wasijihusishe na makundi mabaya mitaani wanaporudi nyumbani kwaajili ya mapumziko mafupi.

“Mnapomaliza mitihani na kurudi nyumbani kunawatu wengi watawatazama na wengine wanaweza kujaribu kuwashawishi ili mjiunge nao hakikisheni mnawaepuka kwani watasababisha mshindwe kutimiza malengo yenu, “ alisema

Wanafunzi wa shule ya St Mary’s Mbagala wakionesha umahiri wa kucheza nyimbo mbalimbali kwenye mahafali ya shule hiyo yaliyofanyika Jumamosi shuleni hapo

“Simamieni na myaendeleze maadili mliyopatiwa na wazazi pamoja na walimu wenu hapa shuleni bado mnasafari ndefu ya kimasomo msije mkabweteka,” alisema.

Aliwataka kutumia elimu waliyoipata kupambana na changamoto za maisha kwani kunachangamoto nyingi na aliwataka wasikubali kukatishwa tama na wakashindwa kutimiza malengo yao.