April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtoto mgongoni ndoo ya karanga kichwani

*Kisa cha Kokusima,miongoni mwa maelfu ya wanawake wanaolea barabarani

Na Judith Ferdinand 

NI saa 2 asubuhi giza linaondoka na mwangaza wa jua unajitokeza juu ya Ziwa Victoria.Upepo mwanana unavuma kutoka ziwani, ukipeperusha harufu ya samaki waliovuliwa usiku kucha. Nipo Kayenze, Kata ya pembezoni mwa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza,nikisubiri kivuko cha MV. Ilemela kinachotoka kisiwa cha Bezi kuja mpaka Kayenze. 

Ninakutana na hadithi ambayo haitoki kwenye vitabu, bali kutoka kwenye maisha halisi ya mama kijana anayejaribu kuokoa familia yake katika kila hatua ya miguu yake.

Mara sauti ya msichana mdogo inanivutia,”karanga za moto!karanga za kuchemsha”.Ninainua kichwa, namuona binti, akiwa na ndoo ndogo kichwani na mtoto mdogo mgongoni(wa miezi 11). Anaonekana mchovu, lakini macho yake yamejaa bidii. Anatembea kwa haraka huku akivuta miguu kwa uzito wa safari yake ya kila siku,ndio! ni safari ya mkate wa kila siku, safari ya matumaini.

Anaitwa Kokusima Mukama (siyo jina lake halisi), ana umri wa miaka 20 tu. Ni mama wa watoto wawili na mke wa mvuvi. Ndio, miaka ishirini,lakini tayari amekumbana na yale maisha ambayo wanawake wengine hukutana nayo wakiwa na miaka 30.

“Sina pa kumuacha mtoto”,katika mazungumzo yetu ya kirafiki kando ya Gati la Kayenze,ambako abiria wanasubili kivuko cha Mv.Ilemela kwa ajili ya kuelekea kisiwa cha Bezi,Kokusima anafunguka kwa unyonge.

“Mume wangu ni mvuvi, wakati mwingine anarudi na samaki wachache sana,na wakati mwingine anarudi mikono mitupu.Nikaamua kuuza karanga ili angalau tupate fedha ya chumvi, unga na sabuni,”.

Kama ilivyo kwa wanawake wengi wa pembezoni, Kokusima analazimika kufanya biashara mtaani huku akiwa na mtoto wake mgongoni kwa sababu hana huduma ya kulea mtoto wala mtu wa kumsaidia.

“Nikitoka asubuhi, lazima nimchukue huyu mdogo. Hata akilala, analala mgongoni. Wakati mwingine anakataa kabisa, analia tu. Lakini sina jinsi, biashara haiwezi kusubiri wala kusimama,”anasimulia Kokusima.

Katika kila hatua anayopiga, Kokusima anakanyaga vumbi la sokoni, anakwepa pikipiki, na mara nyingine anasimama ili kumnyonyesha mtoto mbele ya wateja,ni baadhi ya changamoto zinazowakabili wakina mama kama Kokusima.

Makala hii haimlengi Kokusima pekee,yeye ni sura ya mamilioni ya wanawake walioko vijijini, mijini na pembezoni,wakijitahidi kubeba mzigo wa uzazi, malezi na ujasiriamali kwa wakati mmoja huku changamoto wanazopitia ni nyingi.

Miongoni mwa changamoto ni kutokuwa na uwezo wa kulipia  huduma katika vituo vya kulea watoto mchana (daycare), wanawake hawa hulazimika kubeba watoto kwenye shughuli za biashara kwa kuwa hawana pa kuwaacha, wala uwezo wa kumlipa mlezi.

Mzigo wa kijinsia,kutokana na malezi bado unaonekana kama jukumu la mwanamke pekee katika jamii nyingi hali inayomlazimu mama kufanya shughuli za kuiingizia kipato na wakati huo huo akilazimika kumbeba mtoto mgongoni.

Ukosefu wa muda wa kujipumzisha ambapo wanawake hawa huchoka sana,hawana muda wa kupumzika, na wengi huugua kimya kimya mgongo, shinikizo la damu na msongo wa mawazo.

Hata hivyo watoto walio chini ya umri wa miaka mitano ni waathirika wakuu kutokana na mama zao kufanya biashara wakati wakiwa mgongoni kwa kukosa malezi sahihi.

Katika mazungumzo haya, siwezi kupuuza uwepo wa mtoto aliyeko mgongoni mwa Kokusima.Watoto wa umri huu hasa walio chini ya miaka mitano wanakua katika mazingira magumu sana.Na haya ndiyo matokeo ambayo huenda hayazungumzwi sana.

Kokusima anatazama mbali, anapobonyeza karanga moja mkononi,”Nawaza sana kuhusu kesho yao,watoto wangu wanakua katika ugumu,tazama yule ninaye muacha nyumbani bado mdogo pia miaka mitatu bado hanahitaji malezi ya mimi mama yake.Hata huyu niliyembeba mgongoni hapati nafasi nzuri ya kukua vyema kama watoto wengine ikiwemo lishe bora najua siyo vizuri lakini nifanyeje?,”.

Changamoto za kukosa malezi

Kokusima anasema,katika maisha yake ya kila siku, changamoto za malezi zimekuwa sehemu ya kawaida, lakini si rahisi kuzoeleka.

Anasema,kila siku analazimika kuamka saa kumi alfajiri,muda ambao wengine bado wako usingizini, lakini kwake ndiyo mwanzo wa pilikapilika za kutafuta riziki.

Anaanza kwa kuchemsha karanga biashara yake kuu ya kila siku na baada ya hapo anandaa uji kwa ajili ya watoto wake huku akimsubilia mume wake arejee ili abaki na mtoto wake mkubwa mwenye umri wa miaka mitatu.

“Changamoto huanza pale ninapolazimika kuwaamsha watoto mapema, jambo ambalo najua si zuri kwa afya yao, hasa kwa watoto wa umri mdogo. Lakini sina namna,nawatayarisha harakaharaka, nawapatia uji,saa moja asubuhi nakuwa tayari nimeshatoka kuelekea eneo la biashara ili kuwahi wateja wa asubuhi,”anasema Kokusima.

Anasema kuwa hurejea nyumbani saa sita mchana ili kuandaa chakula cha mchana haraka haraka kisha hurudi tena eneo la biashara akiwa na mtoto mdogo mgongoni,akiwategemea abiria wanaotoka kisiwani Bezi na Ukerewe, au wale wanaoelekea huko.

Wakati mwingine,karanga zikiwa nyingi hulazimika kuvuka maji hadi kisiwani Bezi kwa ajili ya kutafuta wateja huku akiwa na mtoto mgongoni hivyo kurejea nyumbani jioni kuanzia saa tisa hadi saa kumi.

“Wakati huo, mwanangu hulazimika kukaa njaa kwa muda huo mpaka nirejee nyumbani na huyu mdogo hana hata muda wa kucheza na watoto wenzake,muda mwingi yupo mgongoni. Hili linamnyima fursa ya kuchangamka kiakili na kijamii kama inavyostahili kwa mtoto mdogo,”anaeleza Kokusima na kuongeza:

“Nikirudi nyumbani, ninakuwa nimechoka sina muda wa kuwatazama watoto wangu vizuri,wakati mwingine hujisikia huzuni, maana natamani kuwalea watoto wangu kwa upendo, umakini, na muda wa kutosha lakini mazingira yangu hayaruhusu,”.

Changamoto wanazoweza kukumbana nazo watoto wanaobebwa mgongoni wakati wa biashara ni pamoja na kukosa uhuru wa kucheza,ambapo kwa mujibu wa wataalam wa afya watoto huhitaji kucheza ili kukuza ubongo, misuli, uelewa wa kijamii, na kujiamini.

Maoni ya wananchi

“Kubebwa mgongoni muda mrefu huwanyima watoto nafasi ya kucheza, kuchangamana na watoto wenzao, au kujifunza kupitia mazoezi ya kila siku,hali hii inaweza kuchelewesha maendeleo ya kimwili kama kutambaa, kutembea na ya kiakili,”anasema Mukatesi Shukuru mkazi wa wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Kwa upande wake Juma Jumanne, amesema, kutokana na mama kubanwa na muda wa biashara, mara nyingi watoto hawa hawapati muda mzuri wa kunyonyeshwa kwa wale wachanga au kula vyakula vinavyofaa kwa wakati unaofaa.

“Watoto wanaolelewa kwa namna hiyo mara nyingi ujikuta wakiangukia katika lishe duni hali inayoweza kuwasababishia utapiamlo au kukosa virutubisho muhimu katika ukuaji wao, kwani mara nyingi wanajikuta wakipewa chakula aina moja tu,” amesema Jumanne na kuongeza:

“Pia kukosa usingizi wa kutosha kwani watoto wadogo huhitaji kulala muda mwingi wa mchana ili kusaidia ukuaji wa ubongo na miili yao.Hivyo kubebwa mgongoni kwenye shughuli zinazoendelea au kusafirishwa huku na kule huwanyima utulivu wa kulala vizuri,”.

Aidha inaweza kusababisha watoto hao kutohudhuria kliniki na kukosa huduma za msingi za afya kutokana mama kujikita zaidi katika suala la biashara.

Naye Fauster Hugo,anasema,ili kukabiliana na changamoto ya malezi kila mtu anapaswa kushirikiana na kusaidia kulea watoto hao na siyo kumuachia mama pekee yake.

Huku wadau wa maendeleo wakiombwa kuwekeza kwenye huduma za kulea watoto kwa kuweka vituo vya kulea watoto karibu na masoko au maeneo ya biashara ili wanawake waweze kufanya kazi kwa amani.

Hata hivyo Siagi Malinyingi,anaiomba Serikali itoe elimu ya afya na malezi bora kwa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara kina mama kuhusu lishe, huduma za kwanza, afya ya akili na njia mbadala za malezi salama.

Pia iwawezeshe mitaji wanawake wa wajasiriamali ili waweze kuendeleza biashara na hatimaye kumudu gharama za malezi bora kwa watoto wao.

“Mtoto wa chini ya miaka mitano hawezi kujitetea,hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya taifa bila kuwekeza kwenye maisha ya watoto hawa.Hatuwezi kulinda watoto hawa bila kumlinda mama yao,bila kumwezesha mama, hakuna taifa lenye afya wala nguvu ya kesho,”.

Ofisa Ustawi wa Jamii azungumza

Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Pamela Kijazi,anasema kuwa changamoto ya kina mama wanaofanya biashara katika maeneo ya masoko, stendi na mikusanyiko mingine ya watu wakiwa na watoto wao imekuwa ni jambo linalohitaji suluhisho la muda mrefu na endelevu.

Kijazi anasema,kwa muda mrefu, akinamama wengi wamekuwa wakilazimika kuendelea na biashara huku wakiwa na watoto wachanga na wengine wenye umri chini ya miaka mitano,hali inayohatarisha usalama na makuzi bora ya mtoto, pamoja na kupunguza ufanisi wa mzazi katika shughuli za kiuchumi.

Nini suluhisho

Ujenzi wa vituo vya malezi katika masoko na maeneo ya mikusanyiko ndio suluhisho la watoto kupata malezi na wakina mama kupata fursa ya kufanya shughuli za kiuchumi kwa ufanisi.

Kijazi anasema,kutokana na hali hiyo, Serikali kupitia Halmashauri ya Ilemela imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kwamba masoko yote mapya yanayojengwa yanakuwa na vituo maalum vya kulelea watoto mchana.

Anasema,vituo hivyo vitakuwa mahali salama ambapo watoto wataweza,kupata malezi bora kutoka kwa walezi waliobobea,kushiriki michezo,ujifunzaji pamoja na kupata lishe bora kwa afya na ukuaji wa mtoto.

“Kwa watoto wanaonyonya, kutakuwepo na maeneo maalum ya kunyonyeshea.Lengo ni kumuwezesha mzazi, hasa mama mfanyabiashara, kuendelea na shughuli zake huku mtoto akiwa salama na akipata huduma stahiki,”anasema Kijazi.

Mbali na mpango huo wa kujenga vituo vya malezi katika masoko mapya,pia Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wadau ilianzisha vituo vya kulelea watoto katika jamii, ambavyo kwa sasa vipo takribani 17 kwenye mitaa mbalimbali ya manispaa hiyo.

Anasema,vituo hivyo vinapatikana hadi kwenye maeneo ya mialo, ambapo wazazi wengi hujihusisha na biashara ya mazao ya uvuvi.

Huku akisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuwapeleka watoto wao katika vituo hivyo wanapokwenda kufanya shughuli zao za kiuchumi,kwani mtoto anapokuwa kwenye kituo hicho apata ulinzi,chakula chenye lishe bora pamoja na malezi kwa mujibu wa miongozo ya kitaalamu ya malezi na makuzi ya awali ya watoto.

“Mzazi anapomaliza shughuli zake za siku,atamchukua mtoto na kurejea naye nyumbani, kwa mujibu wa utaratibu wa kituo.Natoa wito kwa wazazi wote hasa kina mama wanaofanya shughuli za uchumi katika masoko, stendi, maeneo ya mialo na sehemu zingine zenye mikusanyiko ya watu, watumie huduma hizi zilizopo kwa ajili ya watoto wao,”anasema Kijazi na kuongeza:

“Kwa kufanya hivyo, mzazi atakuwa na uhakika wa usalama na ustawi wa mtoto wake, huku akiendelea kufanikisha malengo yake ya kiuchumi kwa ufanisi zaidi,”.

Jitihada za TAHEA katika malezi ya watoto

Mratibu wa Miradi ya Malezi ya Watoto wa shirika la uchumi wa Nyumbani (Tanzania Home Economics Organization-TAHEA) Mwanza,Damas Joachim,anasema katika kuhakikisha watoto hususani waliochini ya miaka 8, wanapata malezi bora walianzisha vituo vya kijamii vya malezi 12 wilayani Ilemela na sasa wameanza ujenzi wa kituo cha malezi wilayani Misungwi.

Damas anasema,vituo hivyo 12 kwa Wilaya ya Ilemela wamejenga katika mitaa iliopoa katika Kata za Kayenze,Sangabuye,Bugogwa na Shibula kunakofanyika shughuli za uvuvi.

Sababu za TAHEA kuanzisha vituo katika maeneo hayo

Damas anasema,sababu walibaini maeneo hayo hayana mfumo mzuri wa maadili na malezi ya watoto kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wazazi kutojipanga kuanzisha familia au makazi ya kudumu.

“Mtu anaenda kwa lengo za shughuli za uvuvi na kuanzisha makazi ya muda mfupi lakini akifika kule anapata mwanamke wanaanzisha familia kwa kuzaa watoto kitendo ambacho wanakuwa hawajakipanga,hivyo mtu akiona familia imeanza kuwa kubwa anaona bora ajenge na kukaa hapo,katika mazingira ya namna hiyo malezi yanaathirika zaidi,”anasema Damas na kuongeza:

“Pia maeneo ya ziwani mfumo wa maisha hautoi nafasi ya malezi bora kwa watoto kwani muda mwingi wanatumia katika mabanda ya “video”,ata kwenye mwambao wa ziwa unakuta watoto wadogo wenye umri wa miaka miwili mpaka miwili na nusu,wamezagaa katika maeneo hayo na hawana uangalizi mzuri na kule unakuta watu wazima wengine wanaoga hadharani huku watoto hao wakiwashuhudia,”.

Damas anasema,lengo la kuanzisha vituo hivyo vya jamii vya malezi ya watoto wadogo mchana ni kuwapatia watoto wadogo fursa ya kujifunza kwa njia ya michezo (play based learning) ili waweze kupata ukuaji sahihi na kufikia utimilifu wao. 

Pia kuwapa wazazi na walezi muda wa kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zao za uzalishaji mali pasipo wasiwasi wakati watoto wao wakipata malezi mbadala kwenye mazingira salama.

Hata hivyo msingi wa taifa bora ni lenye watoto ambao wanapata huduma ya malezi bora kwa usawa bila kujali hali zao na za wazazi wao.