April 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yafungua duka jipya SGR Dodoma

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKAZI wa Dodoma na maeneo ya jirani pamoja na wasafiri wa treni ya umeme (SGR) wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji rahisi na wa haraka wa huduma za mawasiliano na kifedha kufuatia uzinduzi wa duka jipya la Yas.

Hatua hiyo itakayorahisisha miamala ya kila siku, kuimarisha biashara na kuongeza ushiriki katika uchumi wa kidijitali.

Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, na ni sehemu ya mkakati wa Yas kupanua huduma zake kote nchini ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma za kidijitali karibu nao.

Hatua hiyo inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wafanyabiashara, wanafunzi, wakulima na wajasiriamali, hususan kwa kuzingatia ukuaji wa kasi wa jiji la Dodoma na matumizi makubwa ya usafiri wa SGR.

Akizungumza wakati hafla hiyo, Jabir Shekimweri ameipongeza Yas kwa mchango kwenye uchumi wa kidigitali na uwekezaji unaoendana na kasi ya ukuaji wa jiji la Dodoma.

“Ufunguzi wa duka hili utachochea ajira, shughuli mbalimbali za kiuchumi, kurahisisha maisha ya wananchi na kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu za mawasiliano na kifedha,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas na Mixx, Mwangaza Matotola, amesema kuwa uamuzi wa kufungua duka hilo umetokana na dhamira ya kampuni ya kusogeza huduma karibu zaidi na wateja, hasa katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu kama vituo vya SGR.

“Dodoma ni jiji linalokua kwa kasi na lina mahitaji makubwa ya huduma za kisasa za mawasiliano.

“Kupitia duka hili, tunalenga kuwafikia wateja wetu kwa urahisi zaidi, kuwapa huduma za haraka na za uhakika, na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali,” amesema.

Ameongeza kuwa, duka hilo litatoa huduma mbalimbali za kidijitali na kifedha ikiwemo usajili wa laini mpya, huduma za kifedha kupitia Mixx, ununuzi wa vifaa vya mawasiliano kama router, MiFi na simu janja, pamoja na huduma maalum kama Mjasiriamali Box kwa wafanyabiashara.

“Dhamira yetu ni kuwa mshirika wa kweli wa Watanzania katika safari yao ya mafanikio kwa kutoa huduma rahisi, bora na za kisasa zinazokidhi mahitaji yao ya kila siku,” amesisitiza.

Aidha, Yas imeendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa ikiwemo mifumo ya huduma kwa wateja ya kidijitali kama chatbot, IVR na majukwaa ya mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wateja wanahudumiwa kwa haraka na ufanisi muda wote.

Kampuni pia inajivunia mtandao wake mpana na wenye kasi wa 4G na 5G uliotambuliwa kwa mara tatu mfululizo na Ookla.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TRC Fredy Mwanjala ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TRC, amesema,

“Uwepo wa Yas katika Stesheni hiyo unaimarisha dhana ya stesheni kuwa kitovu cha huduma jumuishi na kuongeza thamani ya uzoefu wa abiria katika ulimwengu wa kidigitali”.

Uzinduzi huu unaongeza idadi ya maduka ya Yas mkoani Dodoma kufikia Matano (05) ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni hiyo wa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuimarisha upatikanaji wa huduma za kidijitali nchini.