April 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kiwango cha utimilifu MSD chapaa hadi zaidi ya asilimia 80

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dodoma

BOHARI ya Dawa (MSD) imepiga hatua kubwa katika kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini, ambapo kiwango cha utimilifu kimeongezeka kutoka asilimia 40 katika kipindi cha miaka minne iliyopita hadi zaidi ya asilimia 80 kwa sasa.

Hayo yamesemwa wiki iliyopita na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, katika semina na wahariri wa vyombo habarí iliyofanyika Ofisi za MSD Kanda ya Kati jijini Dodoma.

Ameoneshwa kufurahishwa na kiwango hicho kwa kuwa,sekta ya afya ni muhimili mkuu wa usalama wa Taifa.

Amesema ustawi wa afya ya jamii una uhusiano wa moja kwa moja na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Tukai aliongeza kuwa jamii isiyo na afya njema haiwezi kuwa salama wala kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

“Afya ni usalama wa Taifa, jamii ikiwa haina afya haiwezi kuwa salama, na bila usalama hakuna uzalishaji, hivyo hakuna uchumi,” amesema.

Amefananisha sekta ya afya na stuli ya miguu mitatu inayojumuisha fedha, huduma na bidhaa, huku MSD ikiwa na jukumu la kusimamia upatikanaji wa bidhaa za afya.

Kwa mujibu wa Tukai, endapo mguu mmoja kati ya hiyo utayumba, sekta nzima itakuwa katika hatari ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Kwa, MSD ina wajibu wa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa bora, salama na zinazowafikia wananchi kwa wakati.

MSD ni kiungo muhimu katika kuhakikisha huduma za afya zinakuwa kamilifu nchini,” alisema na kuongezqa;

“Tunasimamia upatikanaji wa uhakika wa bidhaa za afya. Bila bidhaa hizo, sekta ya afya haiwezi kuwa kamili.Tunahakikisha bidhaa zote ni bora, salama na zinapatikana kwa wakati.”

Ametaja majukumu makuu ya MSD kuwa ni uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya.

Kwa mujibu wa Tukai,MSD inasambaza wastani wa asilimia 81 hadi 83 ya bidhaa za afya katika vituo vya umma, huku kiasi kilichosalia kikitolewa na wadau wengine katika ngazi za mikoa.

Naye mwakilishi wa Wizara ya Afya, Mfamasia Anneth Wilbroad amesema, wizara hiyo inathamini mchango wa vyombo vya habari katika kuelimisha jamii na kuimarisha mawasiliano kati ya sekta ya afya na wananchi.

Mwakilishi wa Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali, Magreth Makilika ameipongeza MSD kwa kuendeleza ushirikiano na vyombo vya habari, akieleza kuwa hatua hiyo ni mfano bora wa uwazi na uwajibikaji katika taasisi za umma.