Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Zaidi ya kaya 20,000 pamoja nabiashara 400 katika visiwa vya Ukerewe, Kanda ya Ziwa, zinatarajiwa kunufaika na huduma ya umeme wa nishati ya jua kuanzia mwezi mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, kufuatia kuelekea kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme wa jua usiotegemea gridi ya taifa (off-grid), unaolenga jamii ambazo kwa muda mrefu zimekuwa nje ya huduma hiyo muhimu.
Rex Energy, kampuni ya uhandisi, ununuzi na ujenzi (EPC) pamoja na utoaji wa suluhisho kamili za nishati ya jua, yenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 ikihudumia serikali, taasisi binafsi, mashirika ya kimataifa, pamoja na wateja wa makazi, biashara na viwanda, inaendelea kutekeleza mradi huo katika visiwa hivyo 10 vilivyo pembezoni kijiographia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Rex Energy, Francis Kibhisa, amesema utekelezwaji wa mradi huo ulifuatia ushindi wa kampuni hiyo katika shindano la Lighting Rural Tanzania, mpango unaohamasisha matumizi ya nishati ya jua nje ya gridi katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Tumeendelea kufanya kazi kwa kasi kubwa katika mazingira magumu yakijiografia ili kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatiadhamira ya serikali ya kupanua upatikanaji wa nishati safi na nafuu,” amesema.
“Kwa sasa tuko hatua za mwisho, na ni faraja kubwa kuona jamii za visiwa hivi hatimaye zitaanza kufurahia umeme wa uhakika kama ilivyo kwa maeneomengine ya nchi. Hili linahusu kurejesha heshima ya maisha, kuboresha kipato na kufungua fursa halisi za maendeleo.”
Mradi huo, uliopatikana kupitia mpango wa ushindani wa Wakala wa NishatiVijijini (REA) unaolenga kuharakisha upatikanaji wa umeme vijijini kupitia nishati jadidifu, umetekelezwa kwa awamu ili kuhakikisha uthabiti wa mifumo na ubora wa huduma.
Wananchi na wafanyabiashara katika visiwa vya Gana, Kamasi, Bwiro na Bulubi wanatarajiwa kuanza kupata umeme ifikapo mwisho wa Mei mwaka huu, huku visiwa vya Kweru Kuu, Kweru Mto, Izinga, Zeru, Bushengere na Sizu vikitarajiwa kuunganishwa ifikapo Desemba 2026, baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za usimikaji.“Kila hatua ya mradi huu imehitaji umakini wa hali ya juu, uvumilivu na malengo thabiti,” ameongeza Kibhisa.
“Tulichagua kwa makusudi utekelezaji wa awamu ili kuhakikisha kila kisiwa kinapata mfumo kamili na unaojitegemea. Kuanzia uzalishaji hadi usambazaji, kila kipengele kimeundwa kukidhi mahitaji maalum ya jamii hizi huku kikihakikisha uendelevu wa muda mrefu.”
Kwa miongo kadhaa, visiwa hivi vimekuwa vikitegemea jenereta za dizeli namafuta ya taa, hali iliyoongeza gharama za maisha, kudhoofisha shughuli zakiuchumi, pamoja na kuathiri utoaji wa huduma katika shule na vituo vya afya,na hivyo kuchochea umaskini.
Kupatikana kwa umeme huu mpya kunatarajiwa kuleta mageuzi makubwa yamaisha kwa kuongeza muda wa shughuli za biashara, kuwezesha uhifadhi wasamaki kwa kutumia majokofu na hivyo kupunguza upotevu baada ya mavunona kuboresha ubora wa mazao, pamoja na kurahisisha matumizi ya nishati safi majumbani.
Shule zitaongeza muda wa kujifunza, huku vituo vya afyavikiboresha uhifadhi wa chanjo na uendeshaji wa vifaa muhimu vya tiba.“Mradi huu unahusisha uwekaji wa mitambo ya sola, mifumo ya kuhifadhi nishati kwa betri, mitandao ya usambazaji, kazi za ujenzi, nguzo za umeme, mita za kisasa, pamoja na kuzingatia viwango vya mazingira chini ya usimamizi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC),”amesema Amebainisha zaidi Kibhisa.
Aidha, Rex Energy imechangia maendeleo ya jamii kwa kuboresha huduma zamaji, usafi na mazingira (WASH) katika Shule ya Msingi Kamasi, ikiwa ni mwanzo wa juhudi pana za uwajibikaji kwa jamii (CSR) katika visiwa hivyo.

“Hadi sasa, tafiti za upembuzi yakinifu, usanifu wa kihandisi, usimikaji pamojana ujenzi wa mtandao wa usambazaji kwa kiasi kikubwa zimekamilika, na mradi umeingia katika hatua za mwisho za majaribio na uunganishaji wa wateja.’’ Ameongeza.
Upatikanaji wa umeme katika visiwa hivi—ambavyo ni mhimili wa uchumi wauvuvi wa Kanda ya Ziwa—unatarajiwa kuongeza thamani ya mazao, kuboresha uhifadhi na uchakataji, kupanua masoko na kuvutia uwekezaji mpya uliokuwa ukikwamishwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.
Aidha, mpango huo unaendana na sera za taifa za nishati safi na usambazaji umeme vijijini, zinazolenga kupanua upatikanaji wa nishati endelevu hukuukipunguza utegemezi wa mkaa na dizeli.
Katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili iliyopita, Rex Energy imekuwa mstariwa mbele kusambaza suluhisho za nishati ya jua nchini, ikiwemo miradiiliyotekelezwa kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumiaWatoto, (UNICEF) na Wizara ya Afya Tanzania, kama vile majokofu ya kiwango cha chini sana cha joto jijini Dar es Salaam na Zanzibar, pamoja na mifumo ya kuhifadhi chanjo kwa nishati ya jua katika vituo vya afya.
Kampuni hiyo pia imeweka mifumo ya sola katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), shule, vituo vya afya na masoko kote nchini.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT