May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mradi wa machimbo ya dhahabu nyanzaga kuanza utekelezaji

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amefanya kikao cha pamoja na Kampuni ya Perseus ya Australia ikiongozwa na Mtendaji Mkuu wake Jaffer Quartamaine kilichojadili kuhusu uendelezwaji wa mradi wa uchimbaji madini ya dhahabu wa Nyanzaga unaomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Ore Corp ambayo hisa zake zimenunuliwa na Kampuni ya Perseus.

Katika Mkutano huo, Waziri Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa kufanikiwa kukamilisha wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuitaka Kampuni hiyo kukamilisha kwa uharaka malipo ya fidia kwa wananchi wanaopisha mradi.

Pia, Waziri Mavunde amewataka wawekezaji hao kuhakikisha wanaanza mapema uendelezaji wa mradi kwa mujibu ya makubaliano ya awali ya kimkataba ili nchi ianze kunufaika na matunda ya utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa dhahabu katika Wilaya ya Sengerema, Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Perseus Bw. Jaffer Quartamaine ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa wakati wote wa mchakato wa ununuzi wa hisa za Kampuni ya Ore Corp na kuahidi kwamba wamejipanga kuanza uendelezaji wa mradi huu mapema kadri iwezekanavyo kutokana na mpangilio wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mradi.

Ameongeza kwamba, kampuni hiyo imejipanga kufanya uwekezaji mkubwa na wa mfano kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kuongeza uzalishaji wa dhahabu nchini.