Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
MKUU wa Wilaya ya Ilala,Edward Mpogolo ,amewataka wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) Mkoa wa Dar es Salaam kuchagua viongozi wenye maadili, uadilifu na uwezo wa kusimamia maslahi ya wafanyakazi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano huo wa uchaguzi, Mpogolo amesema wajumbe wana dhamana kubwa ya kuhakikisha wanapata viongozi watakaoweza kuwatumikia na kutetea maslahi ya wafanyakazi waliowachagua.
Amesema nafasi za uongozi ndani ya TUGHE ni nafasi za utumishi kwa wafanyakazi wa Serikali na sekta ya afya, hivyo viongozi wanaochaguliwa wanapaswa kuwa tayari kuwatumikia wanachama wote kwa usawa.
“Moja ya sifa muhimu za kiongozi ni uwezo wa kuwasaidia na kuwatetea wafanyakazi katika kipindi chote cha uongozi wake. Aidha, kiongozi anapaswa kuwa na maadili mema ili awe mfano mzuri kwa jamii na kwa watumishi anaowaongoza,” amesema.
” Kuna umuhimu wa viongozi kutunza siri za wanachama na watumishi wanaowawakilisha, akieleza kuwa mara nyingi viongozi hupokea taarifa na changamoto mbalimbali zinazohitaji usiri na umakini katika kuzitatua,”amesema

Mpogolo amewataka viongozi watakaochaguliwa kufanya kazi kwa kushirikiana na wenzao na kuzingatia katiba pamoja na kanuni za chama badala ya kufanya maamuzi binafsi.
Amesema viongozi wa TUGHE wanapaswa kuwa daraja muhimu kati ya wafanyakazi na Serikali ili kuhakikisha maslahi ya watumishi yanawasilishwa na kushughulikiwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TUGHE Taifa,Dkt.Jane Madette amesema mkutano huo wa uchaguzi ni sehemu ya utaratibu wa kawaida wa chama unaofanyika kila baada ya miaka mitano kuanzia ngazi ya matawi, wilaya hadi mkoa.
Madette amesema uchaguzi huo unalenga kupata viongozi wapya watakaoendeleza kazi zilizofanywa na uongozi uliopita, huku akisisitiza kuwa mchakato huo ni wa kikatiba na ni sehemu ya utamaduni wa chama.

Naye Mwenyekiti Mpya wa Kamati ya Wanawake Mkoa wa.Dar es Salaam,Dkt.Faraja Kiwanga aliyeshinda katika uchaguzi huo, amewashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumpa kura za ushindi, akiahidi kufanya kazi kwa bidii, uwajibikaji na ushirikiano ili kuimarisha utendaji wa chama na kutetea maslahi ya wanachama.
Amesema ataongoza kwa kuzingatia misingi ya uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji ili kuhakikisha matarajio ya wafanyakazi yanatimizwa katika kipindi chake cha uongozi.

More Stories
Mpogolo: Hali ya usalama Ilala ni shwari
PPAA yashughulikia rufaa 58.kwa mwaka 2025/26
PPAA yashughulikia rufaa 58 kwa mwaka wa fedha 2025/26