May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpango wa Kuzuia na Kukabiliana na Kipindupindu wazinduliwa, Simbachawene asisitiza elimu ya usafi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma 

OFISI ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge na Uratibu imesema kuna mlipuko  wa ugonjwa wa kipindupindu ambapo kuanzia Februari 19 hadi Machi 15 mwaka 2023 imepokea taarifa ya wagonjwa 60 kutoka Mikoa nne ya Tanzania Bara.

 Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Machi 22,2023 Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene kwenye uzinduzi wa mpango shirikishi wa Taifa wa Kuzuia na Kukabiliana na Kipindupindu kabla ya kuuzindua mpango huo ambao umezinduliwa leo.

Kutokana  na hayo Simbachawene ameitaka Ofisi za  Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI),Halmashauri zote kushirikiana na Mamlaka za Maji Mijini na Vijiji (RUWASA) ili kuhakikisha hali ya uaptikanaji wa maji katika maeneo yao inaimarika pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji na kula vyakula vilivyopoa au visivyoandaliwa katika hali ya usafi.

Pia ameitaka Wizara ya afya kuongeza nguvu ya ufuatiliaji ili kuhakikisha wagonjwa na tetesi zote zinatolewa taarifa kutibiwa mapema kwenye vituo vya kutolewa huduma kabla ugonjwa haujasambaa kwenye maeneo makubwa zaidi.

Simbachawene ametaja mikoa yenye wagonjwa wa kipindupindu kuwa ni Ruvuma 1, Kigoma 7, Katavi 34 na Rukwa18.

“Hivi karibuni baadhi ya mikoa kama Katavi, Kigoma, Ruvuma, Manyara na Rukwa imekuwa ikipata milipuko ya Kipindupindu katika baadhi ya Halmashauri zake na kama mnavyojua ugonjwa wa kipindupindu kama yalivyo magonjwa mengine ya mlipuko, unasambaa kwa kasi na wakati mwingine kuvuka hata mipaka ya nchi hivyo lazim kuchukua tahadhari mapema,”amesema Simbachawene 

Vilevile ameeleza kuwa kuna Taarifa kutoka shirika la Afya Dunia inaeleza kuwa na mlipuko mkubwa wa Kipindupindu nchini Malawi ambapo hadi kufikia tarehe 15 Machi 2023 kulikuwa na jumla ya wagonjwa 53,925 na vifo 1,658 vilivyotolewa taarifa.

“Taarifa hii inatupa tahadhari ya mlipuko huo pia kuvuka mipaka na kuingia nchini kwetu hususani pale tusipo imarisha afua mbalimbali za kujikinga na kipindupindu kwa jamii zetu hususani kwa Mikoa inayopakana na nchi hiyo,”amesema.

Aidha amesema kuna tetesi za kuwepo kwa mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu  kwa nchi nyingine tulizopakana nazo kama Msumbiji, DRC Congo, Zambia na Kenya .

“Ni mategemeo yangu kuwa Mikoa hii na Nchi nzima kwa ujumla imejiandaa vyema kuhakikisha kuwa ugonjwa huo kwanza unazuiwa lakini pia unakabiliwa pale utakapokuwa umevuka mipaka na kuingia kwetu,”amesema.

Pamoja na hayo Waziri Simbachawene ametoa wito kwa ngazi zote za utekelezaji kuhakikisha kuwa shughuli zote zilizopangwa kwenye mpango huo zinatekelezwa kwa wakati na weledi mkubwa ili matokeo yake yaweze kuwa chanya katika kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo hatari, hususan kwenye maeneo yenye kupata milipuko ya Kipindupindu mara kwa mara. 

“Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wadau wetu wa maendeleo kuendelea kufanya kazi na serikali katika kutekeleza mpango huu ili kuhakikisha ugonjwa huo unazuia kabisa au kuhakikisha madhara yake yanapunguzwa kabisa”. 

Hivyo basi, ushirikiano wenu unaitajika katika kutekeleza shughuli zote zinazohusiana na kipindupindu kwa kuzikizingatia mpango utakaozinduliwa leo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Jim Yonaz amesema kuwa  mpango huo umeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya Sasa na baadae ili kutokomeza kabisa kipindupindu 

Amesema  Ushirikiano wa kisekta unaitajika katika kutekeleza shughuli zote zinazohusiana na kipindupindu kwa kuzikizingatia mpango utakaozinduliwa na kwamba Serikali inaendelea kusimamia na kuratibu shughuli za kuzuia na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko yakiwemo yale yanayovuka mipaka ya nchi.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa suala la Kuzuia na kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ni mtambuka hivyo Wizara za Serikali, Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali na yale ya Umoja wa Mataifa yanapaswa kishirikiana Kwa ukaribu.

Naye mwakilishi mkazi wa Shirika la Save the children amesema kuwa wamekuwa wakishirikiana na Serikali wanaposikia taarifa ya kuwepo kwa ugonjwa wa kipindupindu na kuweza kutokomeza ugonjwa huo.

“Lengo la Save the Children ni kuhakikisha mtoto analindwa bila kupata madhara yoyote hivyo juhudi zaidi zinahitajika katika  mapambano ya magonjwa ya mlipuko na shirika hili litaendelea kupambana na magonjwa ya hayo kuhakikisha watoto wanakuwa salama na jamii Kwa ujumla,”amesema

Ameeleza njia ambazo shirika hilo linatumia katika kukabiliana na na kipindupindu ambapo moja wapo ni  juhudi za kutoa mafunzo ya mara Kwa mara Kwa watoa huduma ngazi ya Jamii na ufuatiliaji wa kanuni za afya kwa Jamii ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kanuni Bora za afya.

“Tumekuwa tukishirikiana na Ofisi za baadhi ya waganga wakuu takataka ovyo na  kuhimiza wananchi kuepuka kula vyakula vilivyopoa au visivyoandaliwa katika mazingira safi na salama, lengo letu kuhakikisha wananchi wanaacha tabia ya kutiririsha maji ya vyoo kwenye mifereji ya wazi na tabia nyingine hatarishi,”amesema