May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC- awa mbogo kwa walioharibu mindombinu ya maji

Na Israel Mwaisaka, TimesMajira Online, Nkasi

SERIKALI wilayani Nkasi mkoani Rukwa imesikitishwa na kitendo cha watu wasiojulikana  kwenda kuvunja mabomba kwenye chanzo cha maji na kuharibu mfumo mzima wa upatikanaji maji katika kijiji cha Kantawa na kuagiza jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina  ili kuwabaini wale waliofanya kitendo hicho.

Akizungumza na wakazi wa  kijiji hicho mkuu wa wilaya Nkasi Peter Lijualikali alisema kuwa kitendo kilichofanywa na watu hao ni uhujumu uchumi na kuwa hilo halikubaliki na kuwataka wananchi  kutoa taarifa za siri serikalini kama kuna watu wanaowafahamu ambao wametekeleza tukio hilo.

Alisema kuwa mradi huo wa maji umejengwa na serikali  kwa zaidi ya Mil.300 na umekamilika na kuondoa kabisa tatizo la maji katika kijiji hicho na kata ya Kipande lakini anapojitokeza mtu kuharibu miundo mbinu hiyo ya maji ni lazima ashughulikiwe ipasavyo.

Sambamba na hilo mkuu huyo wa wilaya aliendesha zoezi la kupiga kura za siri ambazo zitaviwezesha vyombo vya dola kufanya uchunguzi wake na kuwapata watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria.

Awali diwani wa kata ya Kipande Joseph Mwenda alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa  uharibifu huo wa miundo mbinu toka chanzo cha maji upelekea wakazi wote wa eneo hilo wanaotegemea chanzo hicho cha maji kukosa maji na kuwasababishia usumbufu mkubwa.

Aliiomba serikali kuendelea kufanya uchunguzi  wa kina na wao katika ngazi ya vijiji na kata wataendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wanapata sababu iliyopelekea uharibifu huo ikiwa ni pamoja na kuwabaini wale wote waliotekeleza unyama huo.

Meneja wa RUWASA wilaya Nkasi Shafii Shaban aliomba serikali kwa kushirikiana na Wananchi kuhakikisha watu waliofanya uharibifu huo wanabainika ili kuchukuliwa hatua za kisheria ili liwe ni fundisho pia kwa watu wengine wanaotaka kufanya hivyo na kuwasababishia usumbufu Wananchi.

Alisema kuwa mabomba yaliyokatwa na kuharibiwa toka chanzo cha maji yana thamani ya Tshs,Mil.25

Pia RUWASA ilikabidhi pikipiki kwa chombo cha watumia maji  cha KINTALUNDILO  (CBWSO) kama chombo kitakachoraisisha utekelezaji wa majukumu ya maji.