Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Mbeya
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (MNEC) wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela, amekabidhi matundu 12 ya vyoo kwa ajili ya wanafunzi wa kiume katika Shule ya Sekondari Malama, iliyopo Kata ya Nsalala, wilayani Mbeya Vijijini, ikiwa ni jitihada za kuboresha miundombinu ya elimu.
Makabidhiano hayo yamefanyika Aprili 21, 2026, katika hafla fupi iliyofanyika shuleni hapo, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyotoa miezi miwili iliyopita.
Mwaselela amesema alibaini changamoto ya uhaba wa vyoo wakati wa ziara yake ya awali alipokwenda kukabidhi madawati 200, ambapo alikuta shule hiyo ikiwa na matundu 10 pekee ya vyoo huku ikiwa na upungufu wa matundu 12.

“Nilipokuja kukabidhi madawati, nilikuta kuna matundu 10 ya vyoo huku kukiwa na upungufu wa matundu 12, ndipo nikaahidi kujenga na leo yamekamilika,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali ya CCM inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta ya elimu, na kwamba viongozi wanapaswa kuunga mkono juhudi hizo kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Aidha, ameongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza fedha nyingi katika miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ni wajibu wa viongozi kuwahamasisha walimu na wanafunzi kwa kuboresha miundombinu ya shule.
Katika hatua nyingine, Mwaselela amesema kuwa Aprili 21, 2026 aliahidi kutoa tofali 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa bweni na bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Mwaselela.
Pamoja na hilo, ametoa motisha ya Sh milioni 3.4 kwa walimu na wanafunzi kufuatia matokeo mazuri ya Kidato cha Pili, ambapo wanafunzi 49 walipata daraja la kwanza na wanne daraja la pili.
“Nimetembelea Shule ya Sekondari ya Wavulana Mwaselela, nimetoa motisha na kuahidi kuchangia tofali 5,000 kwa ajili ya ujenzi wa bweni na bwalo, kufuatia matokeo mazuri ya kitaaluma,” alisema.
Mwaselela pia amewataka viongozi wa chama kuendelea kuwafikia wananchi, kusikiliza kero zao na kuzifikisha katika mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Amesema kuwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, Wilaya ya Mbeya Vijijini inapanga kujenga vyumba vya madarasa 724 pamoja na matundu ya vyoo 640.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Malama, Neema Mwakimenya, ameshukuru Mwaselela kwa kukamilisha ujenzi wa vyoo hivyo, akisema hatua hiyo itaboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kiume.
“Hapo awali hali ilikuwa ngumu, tulikuwa na matundu 10 ya vyoo yaliyokuwa yakitumiwa na wanafunzi 429 wa kiume. Sasa ongezeko la matundu 12 limefanya idadi kufikia 22, jambo litakaloboresha hali ya usafi na afya,” amesema.
Ameongeza kuwa juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu zimeongeza hamasa kwa walimu na wanafunzi, hali inayochangia kuongezeka kwa ufaulu shuleni hapo.

More Stories
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni
Mbega ataka viongozi kuimarisha ulinzi kudhibiti wageni.
Kero za Walimu kutoshughulikiwa kwa wakati chanzo Cha msongo wa mawazo-CWT