August 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkenda Apongeza SUZA Kwa Kuzingatia Uchumi wa Buluu



Na Joyce Kasiki, Tanga


WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amekipongeza Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa juhudi zake katika kuendeleza elimu, utafiti na ubunifu unaolenga kuchochea maendeleo, hususan katika masuala ya uchumi wa buluu.


Profesa Mkenda ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la SUZA katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, wakati wa Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.


Akipewa maelezo kuhusu shughuli za chuo hicho, Mkenda alielezwa namna SUZA inavyotumia elimu, utafiti na teknolojia katika kutafuta suluhisho la changamoto za kijamii na kiuchumi, ikiwemo katika sekta zinazohusiana na uchumi wa buluu.


Naibu Makamu Mkuu wa SUZA, Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi, Profesa Abdi Talib Abdalla, amesema chuo hicho kimeshiriki kwa mara ya kwanza katika Tuzo za Watafiti Waliochapisha Matokeo ya Tafiti Zao katika Majarida yenye Hadhi ya Juu Kimataifa, zinazotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Amesema Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA, Mhandisi Dk. Abdulrahim Haroun Ali Suleiman, amefanikiwa kutwaa tuzo hiyo, hatua aliyoieleza kuwa ni ishara ya kuimarika kwa tafiti na uchapishaji wa matokeo ya tafiti za watafiti wa chuo hicho katika majarida ya kimataifa yenye hadhi ya juu.


“Ushiriki wa SUZA katika tuzo hizi kwa mara ya kwanza unaonesha hatua inayopigwa na chuo katika kujenga mazingira yanayowezesha watafiti kufanya tafiti zenye ubora na kuchapisha matokeo yake katika majarida yanayotambulika kimataifa,” amesema Profesa Abdi Talib.


Amesema mafanikio hayo ni hatua muhimu katika safari ya SUZA ya kuimarisha utafiti na kuongeza mchango wa tafiti katika maendeleo ya Taifa.


Katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Profesa Abdi Talib alisema SUZA pia inatambulisha programu mpya za kitaaluma, zikiwemo Shahada ya Kwanza ya Akili Unde na Sayansi ya Data pamoja na Shahada ya Kwanza ya Usimamizi wa Usafirishaji na Uendeshaji wa Bandari.


Aidha, amesema chuo hicho kimeonesha bunifu mbalimbali zinazolenga kutumia teknolojia kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi, ikiwemo mfumo wa uuzaji wa samaki mtandaoni, mfumo wa kugundua changamoto chini ya ardhi, mfumo wa ufuatiliaji wa afya na bunifu za ujasiriamali.


Profesa Abdi Talib amesema ushiriki wa SUZA katika Wiki hiyo unaendelea kukazia nafasi ya chuo hicho katika kuendeleza elimu, utafiti, ubunifu na ujuzi, huku ukionesha namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kutumia maarifa na teknolojia kutengeneza suluhisho na kuchochea maendeleo ya Taifa.