April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mji wa Serikali Mtumba kuwa na miundombinu ya kisasa

Na Mwandishi Uete, TimesMajira Online, Dodoma

MJI wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma umeendelea kuwekewa miundombinu ya kisasa itakayosaidia na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofika katika Ofisi zote zilizopo katika eneo hilo.

Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Bw.Meshack Bandawe akimsikiliza mmoja wa wataalam wa ujenzi wa barabara kutoka Kampuni ya Chico.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Bw.Meshack Bandawe wakati akiongoza kikao cha Timu ya wataalam wanaosimamia ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya Mji wa Serikali inayohusu maji safi na maji taka,umeme, mawasiliano, usalama, ujenzi wa majengo marefu ya wizara awamu ya pili, barabara za lami, zimamoto na uokoaji, gesi na upandaji miti ya matunda.

“Mji wa Serikali hapa Mtumba utakuwa wa kisasa kutokana na miundombinu iliyojengwa na inayoendelea kujengwa hapa kama vile barabara za lami, uwekaji taa za barabarani, majengo ya kisasa na miundombinu mingine itakayoufanya mji huu kuwa na mvuto wa kipekee kama ilivyo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Kwa upande wa miundombinu mingine Bandawe amesema kuwa itawekwa chini ya ardhi ili kuweka mandhari ya mji huo kuwa ya kisasa na ya kuvutia.
Akieleza kuhusu ujenzi wa barabara za lami Bandawe amesema kazi hiyo inaendelea na imefikia zaidi ya asilimia 70 na kazi yakuweka miundombinu mingine inaendelea kama ilivyopangwa.

Katibu wa Kikosi Kazi cha Kuratibu Serikali kuhamia Dodoma na ujenzi wa mji wa Serikali Bw.Meshack Bandawe akiongoza kikao kazi cha kujadili maendeleo na tathmini ya utekeleza wa Mpango kazi wa mradi huo kilichoshirikisha Timu ya wataalam wanaosimamia ujenzi wa miundombinu ya kudumu ya mji wa Serikali inayohusu maji safi na maji taka, umeme, Mawasiliano, usalama, Majengo Marefu ya Wizara awamu ya pili, barabara za lami, Zimamoto na uokoaji, Gesi na upandaji miti na mandhari Itakayojengwa juu na chini ya Ardhi

Ujenzi wa Mji wa Serikali awamu ya pili inatarajiwa kuhusisha ujenzi wa majengo makubwa ya gorofa kwa kila Wizara. Aidha katika mji wa Serikali Mtumba kutapandwa miti ya aina mbalimbali ya matunda.