June 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mix yaendelea kugawa Mamilioni

Na.Mwandishi wetu,Timesmajira

Kampuni ya Mix imesema imeendelea kuhamasisha matumizi ya huduma za kifedha kidijitali kupitia kampeni yake ya “Kila Muamala ni Bahati ya Ushindi”, ambapo hadi sasa imekwishatoa zaidi ya shilingi milioni 35 pamoja na zawadi mbalimbali za vifaa vya Hisense kwa washindi zaidi ya 50.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Biashara wa Mix, James Sumari, amesema kampeni hiyo iliyoanza Mei 2, 2026 na itakayohitimishwa Julai 31, 2026, inalenga kuwazawadia wateja wanaofanya miamala kupitia Mix Super App huku ikichochea matumizi ya huduma za kidijitali nchini.

Sumari amesema washindi wa droo tano zilizofanyika hadi sasa wamejishindia fedha taslimu na vifaa mbalimbali vya Hisense, ikiwemo televisheni, friji za milango miwili na spika. Aliongeza kuwa bado kuna zawadi nyingi za kushindaniwa, zikiwemo safari ya kwenda kushuhudia Kombe la Dunia nchini Mexico na zawadi kuu ya shilingi milioni 50.

Washindi wa kampeni ya “Kila Muamala ni Bahati ya Ushindi” ya Mix, Michael Robert Brayan na Thuweima Bakari, wamesema hawakutarajia kushinda zawadi walizojinyakulia kupitia kampeni hiyo.

Michael, aliyeshinda shilingi milioni moja, amesema awali alidhani taarifa za ushindi wake si za kweli, lakini alijiridhisha baada ya kufika makao makuu ya Mix na kukabidhiwa fedha zake.

Kwa upande wake, Thuweima aliyeshinda vifaa kutoka Hisense, amesema ushindi huo umemfurahisha na kuthibitisha kuwa kampeni ya Mix ni ya kweli na inawapa watumiaji nafasi ya kushinda zawadi mbalimbali.

Washindi hao wameishukuru Mix kwa kuandaa kampeni hiyo na kuwahamasisha Watanzania kuendelea kutumia Mix Super App, wakisema bado kuna nafasi kwa watumiaji wengine kushinda zawadi kabla kampeni haijafikia tamati.