May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mitambo ya kupulizia dawa kuua wadudu zao la pamba kununuliwa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

SERIKALI imesema kupitia bajeti ya mwaka 2023/24 imetenga fedha kwa wakulima wa zao la pamba kwa ajili ya ununuzi wa mitambo itakayotumia Dron ya kupulizia dawa ya kuua wadudu wanaoua zao la pamba.

Hayo yalisemwa jana na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara akiwa katika muendelezo wa ziara yake katika mikoa ya Kanda ya ziwa.

“Wakulima wa pamba walikua wanahangaika kuchukua masaa mengi kufunga madumu mgongoni ili wapulize dawa.”

“Kanda ya ziwa tunahitaji kilimo Cha kisasa Cha umwagiliaji, Rais amefanya mazungumzo na viongozi wenzake Duniani ambapo amepata Dola bilioni 1 itakayokuja kuwekezwa huku na kuwa na kilimo ambacho haijawah kutokea” amesema.

Aidha akizungumza kwa njia ya simu na Makonda, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema Wizara hiyo inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata pamba kati ya simiyu na shinyanga kwa makubaliano ya viongozi na wakulima wakubwa ili kuondoa changamoto ya kuuza pamba kama malighafi, na badala yake kuuza pamba kama bidhaa .

Kuhusu bei ya pamba kushuka, imeelezwa kuwa zao hilo linashuka kutokana na soko la dunia.

Mbali na hayo Makonda amesema chama hakiwezi kukabidhi nchi kwa vyama vingine visivyokubali mabadiliko, ambayo Watanzania wanayahitaji.

“Kuna vyama ambavyo miaka yote viko vilevile, watu wasio kuwa na mabadiliko katika vyama vyao, CCM haiwezi kuwaamini na kuwapa nchi ambayo inahitaji mabadiliko”

“Hakuna chama mbadala zaidi ya CCM, kwani ni chama pekee kinachokubali kujisahihisha, kujikosoa na kukubali mabadiliko, kutokana uhitaji wa wakati huo sawa na ukuaji na maendeleo ya maisha ya mwanadamu, ndivyo chama kinavyo kubali kujibadilisha kutokana na uhitaji ulipo,” amesema.