April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCEA: Wasanii wala ‘unga’lungu kali kuwashukia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) imesema wasanii wote ambao wanajihusisha na dawa za kulevya pamoja na wanaohamasisha utumiaji wa dawa hizo kuacha mara moja kabla kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Hayo yalisema leo jijini Dar es Salaam, na Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Aretas Lyimo wakati wa kuhitimisha semina ya siku mbili kwa Wahariri wa vyombo vya habari.

Lyimo amesema, wanayo orodha ya wasanii mbalimbali wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa hizo na kwamba muda sio mrefu wataanza kuchukua hatua dhidi yao.

Amesema, sheria inawaruhusu kumkamata mtu yoyote ambaye wanahisi anajihusisha na dawa za kulevya, kwenda kumpima na ikithibitika anatumia basi atafikishwa katika vyombo vya sheria.

“Kwa sasa Mamlaka iko katika mchakato wa kuwa na maabara ya kisasa itakayotumika kupima watu wanaohisiwa kutumia dawa za kulevya ili wachukuliwe hatua.

“Tunatarajia kufunga mtambo wa kisasa katika maabara yetu, hivyo tutakuwa na nafasi nzuri ya kukamata wanaohisiwa na kupimwa.

“Pamoja na kuwa na sheria lakini tuliamua kuwa kimya lakini tutakapokamilisha maabara yetu tutaanza kuchukua hatua.

“Mitambo tayari imewasili katika Bandari ya Dar es Salaam na baada ya kukamilisha tutaanza kupima wote wanaohusishwa na dawa za kulevya.

“Baadhi ya wasanii wanahusishwa kutumia dawa za kulevya, niwahakikishe msanii yoyote ambaye anajihusisha na dawa za kulevya tutamkamata na kumpima katika maabara yetu,” amesema Lyimo.

Hata hivyo, Kamishina Jenerali Lyimo amesema Orodha ya wasanii wanaotumia dawa za kulevya wanayo na watakapoanza hawatajali ukubwa wala umaarufu wa msanii yeyote.

Tunawatahadharisha waache kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya,” Tunawafahamu hatutamuacha mtu salama,” amesema Lyimo.

Katika hilo amesema, haitashia kwa wasanii peke yao bali na watu wengine wote ambao wanajihusisha na dawa nao watakamatwa na kupelekwa katika maabara hiyo kwa ajili ya kuchukuliwa vipimo na kama itathibitika kwa namna yoyote ya kutumia dawa za kulevya sheria itachukua mkondo wake.

Ametoa wito kwa Watanzania wote, kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwani Taifa litazidi kudidimia iwapo sula hilo litafumbiwa macho.