April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miradi ya maji Mkinga kunufaisha wananchi zaidi ya 15,000

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Mkinga

Kukamilika kwa ujenzi wa Mradi wa Maji Gombero, utawanufaisha wananchi 10,871 wa vijiji vya Gombero, Vunde Manyinyi, Dima, Jirihini na Kichangani katika Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga na kuweza kupata huduma ya maji safi na salama.

Huku upanuzi wa mradi wa maji Mapatano, utekelezaji wake unafanyika katika vijiji vya Kwangena, Bantu na Machimboni utanufaisha wananchi zaidi ya 4,000.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akitimiza ile dhana ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kumkabidhi ndoo yenye maji mkononi mkazi wa Kijiji cha Bantu Asha Abbas,kushoto ni Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo

Hayo yameelezwa Aprili 13, 2024 na Meneja wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mkinga Mhandisi Thomas Kaijage kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava wakati akiweka Jiwe la Msingi kwenye mradi huo.

Ambapo ameeleza kuwa maeneo hayo ambayo utekelezaji wa mradi wa maji wa Gombero unafanyika yalikuwa yanapata huduma ya maji kutoka mradi wa zamani ambao umekuwa chakavu.

“Ukarabati wa mradi huu unafanyika kutoka chanzo cha maji Mpirani ambacho kipo Kijiji cha Maramba A Kata ya Maramba na ujenzi ulianza Novemba 22, 2022 ulitarajiwa kukamilika Agosti 22, kwa mujibu wa mkataba lakini kutokana na kuchelewa kwa fedha za kumlipa mkandarasi imemfanya kuomba muda wa nyongeza wa utekelezaji, hivyo mradi unatarajiwa kukamilika Agosti 19, 2024,” amesema Mhandisi Kaijage.

Mhandisi Kaijage amesema, lengo kuu la utekelezaji wa mradi huo ni kuongeza eneo la upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi hivyo kuendana na kauli mbiu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ‘kumtua mama ndoo kichwani’.

Amesema utekelezaji wa mradi huo umehusisha kazi ya ulazaji wa miundombinu ya bomba umbali wa kilomita 48.4, ujenzi wa tenki la maji lenye lita za ujazo 300,000, ujenzi wa vituo 28 vya kuchotea maji,ofisi ya CBWSO na banio, ambapo utekelezaji umefikia 56.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akifungua maji kwenye Kijiji cha Bantu katika mradi wa maji Mapatano

Mradi huo utagharimu kiasi cha bilioni 3.15 ambazo ni fedha za Mfuko wa Maji (NWF) unaotekelezwa na Mkandarasi M/S Kings Builders Ltd.

Akisoma taarifa ya upanuzi wa mradi wa maji Mapatano ambao utekelezaji wake unafanyika katika vijiji vya Kwangena, Bantu na Machimboni ambapo maeneo hayo hakuna kabisa huduma ya maji Mhandisi Kaijage ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo ulianza Novemba 23, 2022, na ulitarajiwa kukamilika Mei 23, 2023 kwa mujibu wa mkataba.


Kutokana na kuchelewa kwa fedha za kumlipa mkandarasi, imefanya mkandarasi kuomba muda wa nyongeza wa utekelezaji wa mradi hivyo unatarajiwa kukamilika Mei 14, 2024.

“Utekelezaji wa mradi huu umehusisha kazi ya ulazaji wa miundombinu ya bomba katika umbali wa mita 28,975, ujenzi wa matenki mawili ya maji yenye lita za ujazo 135,000 na 45,000, ujenzi wa vituo 22 vya kuchotea maji na ujenzi wa ofisi ya CBWSO ambapo upanuzi umefikia asilimia 57,”.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava akiweka Jiwe la Msingi mradi wa maji Gombero

Ambapo ameeleza kuwa mradi huo utagharimu kiasi cha bilioni 1.50 ambazo ni fedha za Mfuko wa Maji (NWF), unatekelezwa na Mkandarasi M/S FHS Engineering Co Ltd, na kukamilika kwa ujenzi wa mradi huu utanufaisha wananchi 4,217 wa vijiji vya Bantu, Kwangena na Machimboni kupata huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza kwenye miradi hiyo, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa mwaka 2024 Godfrey Mnzava amesema adhima ya Rais Samia ni kumtua ndoo kichwani mwanamke wa kitanzania, hivyo miradi hiyo ijengwe kwa weledi na kuzingati thamani ya fedha inayopelekwa.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akiwatangazia wananchi wa Kijiji cha Bantu kuchota maji bure kwa siku mbili mara baada ya mradi wa maji Mapatano kutembelewa na Mwenge wa Uhuru Aprili 13, 2024 ambapo RUWASA italipia maji hayo kwa hizo siku mbili
Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo akipanda juu ya tenki la mradi wa maji Gombero, kujiridhisha kabla ya Mwenge wa Uhuru kufikishwa kwenye mradi huo
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mkinga Mhandisi Thomas Kaijage akimuonesha michoro ya mradi wa maji Gombero, Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Godfrey Mnzava.
Tenki la mradi wa maji Gombero lenye ujazo wa lita 300,000