March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mikopo ya halmashauri ilivyowasaidia wenye ulemavu kujikwamua

Na Penina Malundo

KWA muda mrefu watu wenye ulemavu wamekua hawaaminiwi na jamii zinazowazunguka kutokana na kujengewa dhana ya kuwa wao ni watu wa kusaidiwa na kuwa ombaomba.

Ulemavu mara nyingi sio kikwazo cha kumfanya mtu kushindwa kujishughulisha na kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali ili kuweza kulea familia zao, bali baadhi yao wamekuwa wakitumia ulemavu wao kama kigezo cha kukaa na kusubiri kupewa au kuomba kama wanavyofanya wengi.

Ni ukweli usipoingika baadhi ya watu hao wamekuwa wakitumia ulemavu kama sehemu ya kubweteka na kutofanya shughuli yeyote kwa kuona kuwa ulemavu walionao unawakwamisha kufanya shughuli yeyote ya uzalishaji mali.

Kwa kuona hilo Serikali ya Awamu ya Tano iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Dkt,John Pombe Magufuli iliona vema kuanza kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu kupitia Halmashauri za mikoa ili kuweza kuwasaidia kuondokana na wimbi hilo.

Serikali ilitaka kila Halmasahauri nchini kuhakikisha zinatoa asilimia mbili ya mapato ya ndani kwa ajili ya watu wenye ulemavu kupatiwa kama mkopo usiokuwa na riba ambao utawasaidia katika kuendesha maisha yao.

Mbali na kupatiwa mikopo hiyo watu hao wenye ulemavu,pia maofisa maendeleo ya jamii katika kila halmashauri wanatakiwa kulielimisha kundi hilo kuhusiana na mikopo inayotolewa na halmashauri ili iwanufaishe.

Kwa mafanikio makubwa yanayoendelea kuonekana kwa Serikali ya awamu ya Sita sasa, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendeleza kutoa mikopo hiyo kupitia halmashauri mbalimbali nchini na watu wengi wenye ulemavu wameweza kunufaika na kutoa shuhuda mbalimbali walipotoka hadi hapa walipo sasa.

Hakuna haja tena ya watu wenye ulemavu kuendelea kuwa wanyonge kwa sababu Serikali imekwisha kuwakomboa kwa kuwapa mikopo hiyo ambayo pia itawafanya na wao kutegemewa na watu wengine.

Hivyo sasa kupitia mikopo hii inawafanya baadhi ya watu wenye ulemavu kuacha tabia ya kuomba omba mitaani au kukaa barabarani badala yake wajishughulishe kwa kufanya ujasiliamali wa aina mbali mbali kulingana na mahitaji ya sehemu walizo.

Kujishughulisha kutawafanya kuondokana na hali ya kuwa omba omba ambayo tayari serikali imetowa majawabu ya kuwapatia mitaji ya biashara ambavyo wataweza kufanya kwa kupata mikopo kwa njia rahisi.

Na sasa serikali hii ya awamu ya sita imeanza kutoa mikopo kwa watu wenye ulemavu bila hata ya kuwa ndani ya kikundi,hii yote ni kuhakikisha wanawezeshwa na kusimama wenyewe katika kufanya shughuli mbalimbali.

Paipi Lufunguyo(50)Mlemavu wa Miguu anasimulia namna maisha yake yalivyokuwa mwanzo kabla ya kupata mkopo na sasa aasema maisha yake yameweza kubadilika na kuwa tofauti na zamani ambapo hali ya maisha ilikuwa ngumu kutokana na yeye kuwa mlemavu na familia ikiwa inamtegemea.

Lufunguyo anasema halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga imeweza kumsaidia kwa kiasi kikubwa na kumpatia mkopo wa Milioni tano ambao amewa kununua pikipiki mbili na kuanza kuzisimamia.

“Kweli dada… sasa hivi maisha yangu yamebadilika kwa kiasi kikubwa sina tena wasiwasi na maisha kwani tunafanya kazi vizuri na fedha nimeanza kupokea,”anasema na kuongeza

“Nimenunua pikipiki hizo mbili na moja nimempa kijana wangu ambaye kila siku ananiletea 20000 kwa pikipiki zote mbili naweza kupata hata 30000 kwa siku na wakati mwingine hela inazidi kama biashara ikiwa nzuri zaidi na fedha ikizidi upeleka katika shamba langu la Alizeti”anasema

Anasema anamalengo makubwa na pikipiki zake hivyo anahakikisha anazitunza ili aweze kukamilisha kulipa mkopo alipewa na hadi mwezi Disemba mwaka huu.” Nimebadilika sasa na sitaki kuhaibika hata kidogo nimepewa mkopo n halmashauri natakiwa nihakikishe nisirudi nyuma kule nilipotoka mwanzo maisha yangu yalikuwa mabaya sana… sasa hivi nanenepa,”anasema na kuongeza

“Hapa nilipo nalima na shamba la alizeti na mahindi nina heka nne,kihela kikizidi kwenye pikipiki zangu napeleka shambani kidogo,sioni maisha ya kuangaika kama zamani,”anasema

Kwa Upande wake Joseph Mwendapole (45) Mlemavu wa Miguu anasema ulemavu aliokuwa nao ni wakuzaliwa mwaka 1973,ambapo wazazi wake hawakufanikiwa kumpeleka shule kutokana na hali yake.

Anasema alipokuwa na miaka 12 aliamua kwenda Shule mwenyewe na kujitahidi kusoma kwa bidii lakini hakuweza kumaliza shule kutokana na changamoto mbalimbali.

“Nilipokuwa nasoma nilipata changamoto mbalimbali nikiwa mkoani Morogoro ilinibidi nianze kuingia mtaani na kuanza kuombaomba ,nilikuwa naombaomba ili nipate pesa kwaaajili ya kujikimu kimaisha,”anasema na kuongeza

“Nilifanya kazi ya kuombaomba kwa mufa mrefu licha ya kutopenda kazi hii lakini nilikuwa nawaza namna ya kulisha familia yangu,maana nina mke na watoto,”anasema

Anasema ilipofika mwaka 2020 alihama Mkoa wa Morogoro na kuhamia Sumbawanga vijijini na kuanza maisha mapya na familia yake ambapo aliamua kuokoka na kuanza kulima mazao mbalimbali.

“Mimi ni mlemavu ila hali ya kuombaomba ilikuwa inanichukiza sana kwani nilikuwa nahisi nachekwa na kudharaulika na jamii,hali hii inawatokea watu wengi wenye ulemavu utakuta wanaweza kufanya shughuli mbalimbali lakini kutokana na jinsi alivyo anaamua kuombaomba,”anasema

Anaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia ambayo imewasaidia kwa kuwapatia mikopo ili kuondokana na dhana ya kuombaomba.”Serikali imetusaidia mno katika kutupatia mikopo isiyokuwa na riba ambayo tunaweza kufanya shughuli mbalimbali hata biashara na kujipatia fedha,”anasema

Anasema halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga imeweza kumpatia mkopo wa bajaji ambao wameanza kuitumia kuendesha kwaajili ya biashara na kuanza kuongoza maisha yake na familia yake.

Mwendapole anasema kwa sasa anapata kuanzia 30000 hadi 40000 kwa siku fedha ambazo zinaweza kumsaidia kuendesha maisha yake na nyingine kuipeleka katika kilimo.”Kwa kweli tunashukuru sana tunamshukuru Mbunge wetu pia kwa kusimamia hili sisi watu wenye ulemavu kupata mkopo huu bila masharti yoyote na tayari matunda yake tunayaona sasa,”anasema

Anasema hajutii kuwa mlemavu kwani anafarijika kwani kuwa mlemavu sio sababu ya yeye kuwa masikini kwa sababu anauwezo wa kufanya kazi na kupata fedha kama mtu ambaye sio mlemavu.

“Ulemavu ni ule mtu anbaye hana akili lakini mtu akiwa mlemavu sio masikini unaweza ukawa hauna viungo vyote lakini unaakili na uwezo wa kufanya shughuli zako na kuja kufanya vizuri,”anasema

Anasema maisha yake yamebadilika tofauti na miaka ya nyuma na kwasasa sasa kuwa kama mtu ambaye anaviungo vyote vya mwili.

Makamu Mwenyekiti wa SHIRIKISHO la Vyama vya Watu Wenye Ulamavu Tanzania(SHIVYAWATA),Tungi Mwanjala anasema kazi kubwa inayofanywa na Shirikisho lao kuhamasisha wanachama wake kuchangamkia fursa ya mkopo zinazoyolewa na Halmashauri nchini.

Anasema watu wenye ulemavu wamekuwa hasa wa maeneo ya mjini wamechangamkia na kunufaika maisha yao,na baadhi yao maisha yamekuwa mzuri wengine kudiriki kuajiri wasio walemavu kupitia mkopo wa asilimia 2.

“Pamoja na kupata mikopo elimu inahitahika maana mikopo zinatolewa bila elimu watu wenye ulemavu wanajiongeza wenyewe hivyo wakipata elimu Italian kupata fursa wao wenyewe kuweza kujisimamia katika biashara,”anasema

Anasema kwa Watu wenye ulemavu wa vijijini wanaogopa kuchukua mkopo kwasababu ya vitisho mbalimbali wanavyopewa na maafisa wa halmashauri wakishindwa kurejesha watawekwa ndani.

“Watu kama hao wanatakiwa kuwezeshwa kwa fursa zilizopo mfano kilimo cha mpunga Kyela,kokoa,mawese na zinginezo maafisa maendeleo wakawasimamia mwanzo mwisho kwa awamu moja wanaweza wakajifunza na kukomaa vinginevyo vijijini wana hali mbaya tofauti na wa mjini pia mkopo wa asilimia 2 hauna maana kutengwa vijijini,”anasema