April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya sh. bilioni moja kutoka kwa Mfanyabiashara, Rostam Aziz (wa tatu kushoto) ukiwa ni mchango binafsi wa mfanyabiashara huyo wa kuunga mkono mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa jijini Dodoma, jana. Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile,kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Makampuni ya Taifa, Abdulkarim Shah, wa pili ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa Gas, Khamis Ramadhani na kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Said Matamwe (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Michango ya Corona yazidi kumiminika

Na Mwandishi Maalum

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea kutoka kwa wadau msaada wa fedha pamoja na vifaa mbalimbali kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) wenye thamani ya sh. bilioni 6.226. Baada ya kupokea kupokea msaada huo jijini Dodoma jana,

Waziri Mkuu aliwashukuru wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona, ambapo hadi sasa kesi 24 zimeripotiwa tangu kuanza kwa ugonjwa huo nchini na wagonjwa watano wamepona. Waziri Mkuu aliwataka Watanzania waendelee kushirikiana na Serikali katika kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Alisema hadi sasa jumla ya watu 396 wapo kwenye karatini katika maeneo mbalimbali yaliyotengwa wakiwemo wageni wanaoingia nchini ambao wanafuatiliwa afya zao na baada ya siku 14 kama watakuwa hawana maambukizi wataruhusiwa kuungana na familia zao.

Waziri Mkuu alisema Serikali kwa upande wake imeendelea kuchukua mbalimbali katika kupambana na ugonjwa wa COVID-19 na kwa sasa imejiimarisha kwenye utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na virusi vya corona.

“Serikali inatoa misitizo kwa wananchi wazingatie maelekezo yanayotolewa kuhusu kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona ikiwemo kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka pamoja na kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.”

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ili kuzuia usisambae kwa sababu hadi sasa mkoa huo unaongoza kwa kuwa na wagonjwa zaidi wa corona nchini. Pia, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuvishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na virusi vya corona

pamoja na wasanii waliotunga nyimbo za kuuelimisha umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Miongoni mwa wadau waliotoa msaada huo ni kampuni ya Madini ya Twiga iliyotoa sh. bilioni nne, mfanyabiashara maarufu nchini Rostam Aziz ametoa sh. bilioni moja, kampuni ya Taifa Gesi imetoa sh. milioni 100 na kampuni ya mafuta ya Puma imetoa msaada wa mafuta lita 50,000 zitakazotumika katika magari yanayotoa huduma za kupambana na corona nchini yakiwemo magari ya kubebea wagonjwa.

Wengine ni kampuni ya TEHAMA ya Huawei ilitoa vifaa kuendeshea mikutano kwa njia ya video ambavyo ni cloudlink camera tatu, Cloudlink Mic tatu, Cloudlink TV terminal tatu, Cloudlink Platform pamoja na Thermal Imaging Temperature Measuring System sita vyote vikiwa na thamani ya sh. milioni 940, Asasi za Kiraia (AZAKI) zimetoa sh. milioni 79.

Baada ya kupokea misaada hiyo, Waziri Mkuu kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli aliwashukuru wadau hao kwa vitu mbalimbali walivyovitoa kwa ajili ya kupambana na COVID-19 kwani vifaa pamoja na fedha walizozitoa zitaisadia Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Kuhusu wadau wengine wanaohitaji kutoa misaada, Waziri Mkuu amesema ofisi yake iko wazi pia wanaweza kupeleka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kwa walio nje ya nchi au sehemu yoyote wanaweza kutuma fedha kupitia akaunti Na: 9921159801 yenye jina la National Relief Fund Electronic.

Awali, mfanyabiashara maarufu nchini, Rostam Azizi alisema ametoa sh. bilioni moja ambayo ameielekeza katika kununua vitakasa mikono ambavyo vitatumiwa na wasafiri wa daladala wa Dar es Salaam na Zanzibar ili waweze kutumia kabla ya kupanda usafiri huo, hivyo kuweza kujikinga. Pia, Mfanyabiashara huyo alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwaongoza

Watanzania kwa hekima na busara na kuwaepusha na taharuki kama ilivyotokea katika mataifa mengine.

Amempongeza Waziri Mkuu na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa namna wanavyoshiriki katika kukabiliana na Corona.

Wakati huo huo, Ubalozi wa China nchini umeipatia Serikali msaada wa vifaa kinga kwa ajili ya kuendelea kupambana ya ugonjwa wa Corona na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kukabiliana na ugonjwa huo hadi hapo utakapomalizika.

Akipokea vifaa hivyo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu alisema msaada huo utaenda kwa watumishi wa afya kote nchini, kwani Serikali imetoa kipaumbele cha kwanza kwao ili kuwakinga na maambukizi ya Corona.

Waziri Ummy alisema msaada huo uliotolewa na ubalozi wa China nchini ni pamoja na mavazi (PPE) 1,000 ya kujikinga wakati wa kuhudumia watu waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Corona, Barakoa (Mask) 100,000 pamoja na vipima joto vya mkono (thermal scanner) 150.

tunaishukuru sana Serikali ya China kwa mchango huu, na niendelee kuwathibitishia wale wote mnaoisaidia Serikali ya Tanzania msaada huu tutaupeleka kwa watumishi wa afya, kipaumbele ni kuwakinga watumishi wa afya wasipate maambukizi,”alisema Waziri Ummy

Kwa upande wake Balozi wa China nchini Tanzania,Wang Ke alisema nchi yake na Tanzania ni marafiki kwa muda mrefu na ugonjwa huo ulipoikumba Nchi yao kwa mara ya kwanza, Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono katika mapamabana dhidi ya ugonjwa huo, hivyo na wenyewe wamejitoa kuisaidia kukabiliana nao.

Wang Ke alisema Serikali ya China kwa sasa imechukua hatua na kujitoa rasmi kuwa nchi itakayoisaidia Tanzania katika misaada ya dharura ya vifaa kukabiliana na ugonjwa wa Corona

Katika mwendelezo wa kuisadia vifaa kinga Serikali ya Tanzania, kwa mara nyingine tena inatarajia msaada wa vifaa tiba vya kusaidia  wagonjwa kupumua (Ventilator) 500 kutoka kwa mfanyabiashara raia wa China Jack Ma.

Katika  hatua  nyingine, Waziri Ummy amethibitisha kuwepo kwa mgonjwa mpya wa Corona jijini Dar es Salaam. Taarifa iliyotolewa na Waziri Ummy jana mgonjwa huyo ni mwanaume mwenye umri wa miaka (51) raia wa Tanzania, mkazi wa Dar es Salaam.

Mgonjwa yuko chini ya uangalizi wa watoa huduma za afya katika kituo maalum cha tiba Dar es Salaam. Taarifa hiyo ilieleza kuwa Wizara ya Afya inaendelea kuwafuatilia watu wa karibu (contacts) waliowahi kukutana na mgonjwa huyu.

Hivyo, hadi sasa jumla ya watu (25) wamethibitika kuwa na maambukizi ya COVID-19 tangu kuanza kwa ugonjwa huu nchini.