April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia yapaisha Tanzania kidiplomasia

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

MIAKA mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa na mafanikio makubwa katika eneo la kidiplomasia na kuletea Taifa mafanikio katika eneo la kiuchumi, uwekezaji na biashara.

Hayo yamesemwa na Balozi John Ulanga, kwenye kongamano la miaka mitatu ya Rais Samia lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa ya Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam jana.

Ametaja eneo la kwanza ni mahusiano ya nchi na nchi, ambapo amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Samia ameweza kuelekeza kufunguliwa ofisi mpya mbili za ubalozi, ambazo hazikuwepo Jarkata, Indonesia.

Amesema Indonesia ni moja kati ya nchi zinazokua sana kiuchumi. Alitaja ofisi ya pili kuwa ni ni Viena, Austria.

Mafanikio mengine ni nchi ya Denmark kufuta uamuzi wao wa kufunga ubalozi wake nchini Tanzania miezi michache baada ya Rais Samia kushika madaraka ya urais.”Amesema Balozi Ulanga.

Denmark walitoa tangazo la kufuta ubalozi wao Tanzania wakati Rais Samia anaingia madarakani, lakini sasa wameamua kurejesha mahusiano yao kwa kufuta uamuzi huo.

Amesema kufunga ubalozi haukuwa uamuzi mzuri kati ya Denmark na Tanzania, lakini sasa hali hiyo imekaa vizuri kutokana na nchi hiyo kurudisha mahusiano na nchi nchi yetu.

Aidha, ametaja mafanikio mengine kuwa ni uhusiano mzuri wa nchi na nchi ambayo yamechangia ujio wa viongozi wengi wa kimataifa, kuja Tanzania kikazi.

Naye Mhandisi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Mwanaasha Tumbo, amesema Rais Samia alipoingia tu madarakani alihakikisha mkakati wa mazingira ya mabadiliko ya Tabianchi unakamilika.

“Na hilo likiwa ni lengo kwamba tuweze kutekeleza sasa zile sera zote zilizopo. Na huu mkakati upo ukiangalia kwenye mtandao mtaupata,”amesema na kuongeza;

Hiyo tu haitoshi, kwa mujibu wa mikataba ya Kimataifa kila nchi inatakiwa ieleze inaenda kusaidiaje katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi.”

Aidha, amesema tayari kuna taasisi ya kituo kinachosimamia masuala la Cabon kilichopo Chuo cha Sokoine. Lakini pia, amesema kanuni ya kusimamia biashara hiyo nayo tayari imeandaliwa tangu mwaka 2022.