April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Masauni ampongeza Rais Samia kwa kuongeza idadi ya Polisi

Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline,Kilimanjaro

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo ameviwezesha vyombo vya ulinzi kuongeza idadi ya askari ambao wanaimarisha ulinzi na usalama nchini.

Hayo ameyasema juzi Mjini Moshi katika Shule ya Polisi Tanzania wakati akifunga mafunzo ya awali ya askari Polisi katika kambi ya Kilele Pori Wilayani Siha, Mkoani Kilimanjaro.

Mhandishi Masauni amewataka askari hao kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi na amewahimiza kuwa mfano kwa askari watakao wakuta katika mikoa na vituo vya kazi watapopangiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi.

Kwa upande wa Kamishna wa Polisi, Fedha na Logistiki, Liberatus Sabas, ambaye amemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini aliwataka askari hao wapya kutambua kuwa askari ni kioo cha jamii, ambapo amewataka kwenda kutatua changamoto za wananchi wanaolitegemea Jeshi hilo.

Kamishna wa Polisi Operesheni mafunzo wa Jeshi la Polisi CP, Awadhi Juma Haji alibainisha kuwa mafunzo ya kijeshi yanahitaji uvumilivu na nidhamu kubwa ili uweze kufaulu mafunzo hayo, ambapo alisema wataendelea kuwafundisha askari hao wakiwa kazini ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji.

Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Ramadhan Mungi alisema askari hao wamefundishwa mambo mengi, ambayo yamewajenga kitaluma na kijeshi, huku alibainisha kuwa wapo wanafunzi ambao wamefukuzwa mafunzo kwa kutokidhi viwango vya Jeshi hilo ambao Jumla yao ni 193.