May 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Miaka 7 ya BMH:Mkurugenzi aelimisha kuhusu Bima ya Afya kwa wote

MIAKA 7 YA BMH: MKURUGENZI AELIMISHA KUHUSU  BIMA YA AFYA KWA WOTE

Na. Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano Hospitali ya Benjamin Mkapa.

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa,Dkt. Alphonce Chandika amewajengea uwelewa juu ya Mswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote wananchi waliyofika kupata huduma ambapo amesema  lengo la Mswada huo ni kuhakikisha, kila mwananchi anakuwa na uhakika wa kupata matibabu bila hofu.

Dkt.Chandika ametoa elimu hiyo jijini Dodoma leo Oktoba 13 katika Hospitali hiyo ambapo leo imetimiza miaka saba tangu ilipoanza kutoa huduma za Afya Oktoba 13, 2015.

“Ndugu zangu baadhi yenu mnakuja hapa mara kwa mara kupata huduma, mnafahamu ugonjwa haubishi hodi, bila kuwa na BIMA kuna wenzetu hulazimika kuuza hata viwanja au nyumba wagharamie matibabu” Alidokeza,Dkt. Chandika.

Aidha, amefafanua kuwa mantiki ya Mswaada wa BIMA ya Afya kwa wote ni kuhakikisha kuwa, watu wengi wanachangia gharama za matibabu kabla hawajafikwa na maradhi ili kutunisha mfuko hatimae mtu akiugua asikutane na changamoto yoyote ya kukosa huduma kwa kushindwa kulipia gharama za matibabu.

“Msingi wa BIMA ya Afya kwa wote, ni suala la upendo zaidi, na baba wa Taifa Mwalimu Nyerere tunaeadhimisha  siku yake kesho alitufundisha kupendana, hivyo tunapochangia wengi, wakaugua baadhi tunakuwa tumewasaidia”Amefafanua Dkt. Chandika.

Vile vile, ameeleza kuwa mapendekezo ya Mswada huo ni kwa kaya moja kuchangia Shilingi 340,000 na kunufaisha wanafamilia sita, huku mtu mmoja akitakiwa kuchangia kiasi cha shilingi 84,000 ili kupata huduma za Afya kwa mwaka mzima.

“Nasisitiza kuwa serikali haina lengo la kumlazimisha mtu kuchangi, bali itaweka mazingira rafiki yatakayomsukuma kila mmoja kuona umuhimu wa kuchangia, na kwa kutumia mifumo ya TASAF na Ustawi wa jamii itawatambua wasiyojiweza na kuwatengenezea mfumo wa kupata matibabu bila usumbufu”amesema Dkt. Chandika.

Shamrashamra za kutimiza miaka hiyo saba zimeanza saa mbili asubuhi ya leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo Dkt. Alphonce Chandika kushiriki kutoa huduma za msingi kwa wagonjwa, aliwapokea, kuzungumza nao na kuwasaidia waliyohitaji kutembea kwa msaada wa kiti maalumu (Wheelchair).

Pamoja na hayo Dkt.Chandika aliwashukuru wananchi waliyofika Hospitalini hapo kwa kutoa mchango wao wa maoni, ambayo hupokewa na kufanyiwa kazi kwa wakati na ndiyo umekuwa msingi wa maboresho mbalimbali ya huduma katika Hospitali hiyo kiasi cha kuifanya kutambuliwa kama kinara kwa Utoaji wa huduma bora za Afya kwa Hospitali zote nchini.

Awali sherehe hizo zilisindikizwa na ukataji wa keki  maalumu ya miaka saba ya huduma katika Hospitali hiyo, ambayo ilikatwa kwa ushirikiano wa Mteja na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo.

Baadaye alielekea katika wodi ya watoto wachanga na kutoa zawadi mabalimbali kwa watoto hao kama sehemu ya kurejesha kwa jamii.