December 6, 2021

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgeja ajitokeza kupata chanjo ya UVIKO-19,wanaopotosha ukweli washtakiwe

Na Suleiman Abeid,TimesMajira Online,Shinyanga

SERIKALI imeshauriwa kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaopotosha ukweli kuhusu chanjo ya kujikinga na gonjwa hatari la UVIKO 19 upotoshaji ambao unaweza kusababisha watu wengi kupoteza maisha.

Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati akizungumza na wakazi wa Shinyanga katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Ofisi yake, muda mfupi kabla ya uzinduzi rasmi wa chanjo ya UVIKO 19.

Ushauri huo umetolewa mjini Shinyanga na Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation, ya Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja muda mfupi baada ya kuchanjwa chanjo ya kinga ya UVIKO 19.

Amefafanua mwenyekiti huyo alisema watu wanaopotosha ukweli kuhusu chanjo hiyo wamekuwa wakiwajaza hofu wale ambao wana nia nzuri ya kuitikia wito wa Serikali ikiwataka wananchi kujitokeza kupatiwa chanjo kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa huo.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ya mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akichanjwa chanjo ya kinga ya UVIKO – 19

“Binafsi nafikiri ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kukunjua makucha yake kwa hawa wanaopotosha kuhusu hii chanjo ya UVIKO 19, ni vyema wakaanza kuchukuliwa hatua za kisheria, maana wanapotosha watu pasipo sababu,”

“Hawa ki uhalisia hawana tofauti yoyote na magaidi wakubwa duniani, dhamira ya magaidi wakati huo huwa ni kutaka kuchafua hali ya amani na utulivu kwenye nchi zenye utulivu na inapotokea hivyo lazima patokea mauaji mengi, sasa hawa wanaopotosha hawana tofauti na magaidi, maana wanataka watu wafe,” ameeleza Mgeja.

Ameendelea kueleza kuwa iwapo kweli wapotoshaji hao wangekuwa na dhamira ya kweli kutaka kuonesha madhara ya chanjo inayotolewa hivi sasa nchini kote, basi wangekosoa kitaalamu, kwa vile mambo ya kitaalumu hukosolewa kitaaluma vile vile.

Kutokana na wao kushindwa kuwaeleza kitaaluma atanzania madhara yanayoweza kupatikana kutokana na chanjo hiyo ni vyema sasa wakosoaji hao wangekaa kimya na waache upotoshaji wanaoufanya hivi sasa ili kuepusha watanzania wengi watakaokubaliana na upotoshaji wao wasipoteze maisha pasipo sababu.

“Mimi leo hii nimeitikia wito wa Serikali na nimekuwa miongoni mwa wakazi wengi wa mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kuja kuchanja chanjo hii, nimechanja, niwaombe na wengine wote ambao hawajajitokeza wajitokeza mapema wachanje ili wapate kinga kuepuka kupatwa na ugonjwa huu,” ameeleza Mgeja.

Katika hatua nyingine Mgeja amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali chanjo hiyo kuingizwa hapa nchini ili watanzania waweze kuchanjwa kwa lengo la kunusuru maisha yao ambapo pia amempongeza mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Dkt. Philemon Sengati kwa juhudi anazozifanya katika kuhamasisha.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation ya mjini Kahama mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) baada ya kupatiwa chanjo ya kinga ya UVIKO 19.

Naye mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Philemon Sengati akizungumza katika uzinduzi wa chanjo hiyo amewaomba wakazi wote wa mkoa wa Shinyanga wajitokeza kwa wingi kupatiwa chanjo hiyo ambayo inatolewa kwa lengo la kuwezesha mwili kutengeneza kinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19.

Dkt. Sengati amesema chanjo ya UVIKO 19 ni salama kutokana na kufanyiwa uchunguzi wa kina na wataalamu wa afya wa hapa nchini ambapo amewaomba wananchi na kutoa wito wawapuuze wale wote wanaopita mitaani wakipotosha kuhusu ukweli wa chanjo hiyo.

“Ndugu zangu leo na sisi wakazi wa mkoa wa Shinyanga tumeanza kupatiwa chanjo hii ya kinga ya UVIKO 19, katika mkoa wetu tumepokea dozi 25,000 zitakazotolewa kwenye vituo 18 vilivyopangwa rasmi kwa kazi ya kutoa chanjo. Chanjo hii itasaidia kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona,” ameeleza Dkt. Sengati.