April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mgao wa Samatta Simba na kamati nyingi za Yanga

Na Philemon Muhanuzi

PICHA za Mbwana Samatta akiwa kule Uingereza zinamuonyesha akiwa ni mwenye furaha, kavaa koti zuri na kichwani kavaa kofia ya baridi, mikono mfukoni kasimama anaitazama kamera.

Kipindi cha Corona anajifungia ndani na akitoka nje mwisho wake ni eneo la mpaka wa nyumba anayoishi. Lakini sio yeye peke mwenye kulazimisha taswira ya furaha katika siku hizi za watu kuvaa barakoa.

Wanasoka wa vilabu vikubwa kila wakiamka, wanawasha vinakilishi mpakato vyao au simu za mikononi na kuanza kujuliana hali kiujumla.

Aliye mgonjwa kati ya watu wa benchi la ufundi anajulikana wakati wa maongezi ya timu nzima. Aliye mgonjwa miongoni mwa wachezaji nae anakuwa amepata fursa ya kutambulika mbele ya wenzake wote.

Burudani inayoendelea mtandaoni ipo miongoni mwa wapenzi wa timu ya Liverpool, wanapoamka kocha wao mkuu Mjerumani Jurgen Klopp huwasamilia na kutaniana nao kama vile hakuna janga la Corona.

Anamuuliza kila mchezaji kupitia mawasiliano ya kioo cha kinakilishi chake kama ameamka salama, ukizingatia kuwa anamuona kila mmoja wao.

Ligi ambayo Liverpool wanaongoza katika msimamo kabla ya maradhi ya Corona ndio hiyo hiyo ambayo Aston Villa anayochezea Mbwana Samatta inashiriki.

Huwezi kuuita ni ligi kuu ya kitoto na Samatta hajafikia viwango hivyo kwa uchezaji wa bahati nasibu.

Kinachoweza kukushangaza unapokuwa ni mmoja wa washiriki wa mijadala ya makundi sogozi ya soka (Whatsapp), ni pale unapoona masikhara miongoni mwa wanasimba na wanayanga namna wanavyomuongelea Samatta katika lugha ya kejeli.

Ni hoja ya kishabiki inayoikejeli Simba ikitoka kwa Wanayanga, pale wanapouliza yale malipo ya mgao wa Simba katika mauzo ya Samatta kutoka Genk kwenda Aston Villa kama yameshalipwa.

Wanayoishadidia hoja hii ya Simba kuonekana kutopata chochote kwa maana ya pesa ya maana kuingia katika akaunti za benki ni Wanayanga, wanaongozwa na ushabiki.

Lakini wanayo mengi ya kutakiwa kuzitafakarisha akili zao kwani Mbwana Samatta mpya anaweza kuwa ni sehemu ya kikosi cha vijana cha Yanga cha leo hii.

Naitazama Yanga ikiwa na rundo la wanachama wenye nafasi za kiuongozi ndani ya klabu yao. Hawa ni wajumbe wa mkutano mkuu, mahali ambapo panawapa sifa ya kuwa watendaji wakuu wa shughuli za kila siku za klabu.

Wanapewa vyeo vya kila aina na majina yao huwa yanatajwa kwa mbwembwe katika zile dakika za taarifa za habari zinazotengwa mahsusi kwa ajili ya michezo.

Hawa ni wajumbe wa kamati mbalimbali, ambazo kiutaratibu ndizo zenye kuiendesha Yanga. Nani anayesimamia utendaji kazi wao ndani ya hizo kamati?.

Kama wamefaulu kuacha kumbukizi ya maana au yameshindwa, nani mwenye kuweza kuueleza umma kwa maana ya kurudisha mrejesho wa vikao vilivyowapatia nafasi hawa wajumbe wa kamati?.

Hizi kamati zinafanana na majukwaa ya kuyauza majina ya wajumbe miongoni mwa wanajamii wapendao soka. Mtu anafurahia kuwa mjumbe wa kamati fulani ya Yanga, lakini nani anayepima ufanisi wa ujumbe wake?.

Kama klabu yenye mamilioni ya mashabiki na maelfu ya wanachama halali inashindwa kuwaandaa wachezaji kadhaa wa viwango vya dunia kila mwaka, hapo lipo tatizo la msingi ambalo ni kubwa kuliko wapenda soka wanavyodhani.

Simba haina mgao kutokana na mauzo ya Mbwana Samatta kutoka Genk kwenda Aston Villa. Pengine Simba ilipata mgao wa mauzo kutoka TP Mazembe kwenda Genk.

Na wakati Samatta anaonyesha ubora wa kuja kuuzwa kimataifa, pengine Simba ilikuwa na kamati nyingi kwa idadi kuzidi zile za Yanga.

Kulikuwa na minyukano ya kihulka miongoni mwa wanachama, iliyosababisha baadhi ya kufukuzwa.

Utamaduni wa kiuongozi ndani ya vilabu hivi viwili nchini umeendelea kuwa hivyo licha ya Samatta kuweza kupata soko kutokana na nidhamu yake binafsi.

Wanahitajika watu wenye weledi mkubwa kupewa nafasi za kuwa wanakamati wa hizi kamati za Simba na Yanga.

Kama wataendelea kupatikana hawa wajanja wajanja wenye nia za kibinafsi kama wajumbe wa kamati za Simba na Yanga, hakutaweza kuonekana tija inayotarajiwa.

Zitaundwa kamati nyingi tu na wajumbe ni wale wale wapenda soka wenye kuutizama mchezo kijuujuu tu pasipo ule moyo wa kutaka kuutumikia mchezo kwa dhati ya ndani kabisa ya moyo.

Ni kweli mgao mauzo ya Mbwana Samatta kutoka Genk kwenda Aston Villa yanaweza yasiwe na faida katika mipango ya Simba lakini ni kweli pia kamati nyingi za Yanga na vilabu vingine zinaweza kuwa zinaundwa kama fasheni tu.

Simba na Yanga zikikosa watu wa kweli wa mpira walio na utayari wa kuzitumikia, na tuwe tayari kuwa watazamaji wa maendeleo ya vilabu vya mataifa makini kisoka.