March 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii Ruth Minja

Mfumko wa bei wasalia kama ilivyokuwa Mwezi Septemba

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

MFUMKO wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba  mwaka huu umebaki kuwa asilimia 4.0 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu .

Akizungumza leo na waandishi wa habari katika ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS),Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii kutoka NBS Ruth Minja amesema kuwa,hiyo inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu.

Aidha amesema,Mfumko wa bei kwa mwaka ulioishi mwezi Oktoba mwaka huu kuwa sawa na mfumko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu umechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa mfumko wa bei wa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Oktoba mwaka  2021 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba mwaka 2020 .

“Kwa mfano baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonyesha kupungua kwa mfumko wa bei mwezi Oktoba 2020 ni pamoja na maharagwe,kwa asilimia 5.5,dagaa kwa asilimia 3.9,naziwa ya ng’ombe kwa asilimia 5.1 na choroko kwa asilimia 2.3.”amesema na kuongeza kuwa

“Kwa upande mwingine bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kuongezeka kwa mfumko wa bei kwa mwezi Oktoba 2021 zikilinganishwa na bei za mwezi Oktoba 2020 ni pamoja na mavazi kwa asilimia 4.8 ,gesi ya kupikia kwa asilimia 2.8,mkaa kwa asilimia 3.9 na gharama za malazi kwenye nyumba za kulala wageni kwa asilimia 5.7.”amesema Minja

Kwa Mujibu wa Minja ,mfumko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba 2021 umepungua hadi asilimia 3,9 kutoka 4,0 kwa mwaka ulioishia mwezi septemba 2021.

Aidha amesema,mfumko wa bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Oktoba 2021 umebaki kuwa asilimia 4.1kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba mwaka huu.

Kuhusu hali ya mfumko wa bei kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Oktoba mwaka huu amesema,kwa nchi ya Kenya mfumko umepungua hadi asilimia 6.45 kutoka asilimia 6.91 kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2021,

Kwa nchi ya Uganda amesema,mfumko wa bei katika kipindi hicho umepungua hadi asilimia 1.9 kutoka asilimia 2.2.