Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Evance Bisesagu (47), mfanyabiashara na mkazi wa Bupumula, Kata ya Nyamh’ongolo, wilayani Ilemela, kwa tuhuma za kuchimba mahandaki sita na kufanya shughuli za ujenzi wa nyumba ya makazi bila kufuata taratibu za kisheria.
Mtuhumiwa huyo, ambaye ni mmiliki wa jengo hilo, amekamatwa Aprili 22,2026 majira ya jioni kufuatia taarifa za wananchi kuhusu uwepo wa mahandaki hayo yanayohatarisha usalama wao.

Akizungumza mkoani hapa,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbord Mutafungwa, amesema baada ya ufuatiliaji wa kina imebainika kuwa mtuhumiwa alikuwa akijihusisha na shughuli za ujenzi wa mahandaki bila kuwa na vibali vyovyote kutoka mamlaka husika, wala kutoa taarifa kwa mamlaka za kisheria.
Pamoja na mmiliki huyo,pia jeshi hilo linawashikilia watu wengine wawili ambao ni Ngasa Kasuka na Hamad Juma Kashinje, ambao ni vibarua, waliokuwa wakishiriki shughuli za ujenzi katika eneo hilo huku msako ukiendelea kuwatafuta mafundi na watu wengine waliokuwa wakishirikiana nao.

Hata hivyo alitoa rai kwa viongozi wa mamlaka mbalimbali za Serikali kufuatilia kwa kina mienendo ya watu wanaoishi katika maeneo yao ili kujiridhisha na usalama.
Vilevile, kwa ujenzi wowote unaofanyika katika mitaa hiyo, mamlaka zinazohusika na ujenzi zinatakiwa kuhakikisha kuwa vibali vinazingatiwa.Na yeyote atakayebainika kujenga bila vibali, shughuli hizo lazima zisitishwe.


More Stories
Silinde azindua baraza la sita la Wafanyakazi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji
NMB ilivyosaidia Serikali kukusanya zaidi ya Sh trilioni 9.8
Serikali yaongeza nguvu kwa wachimbaji wadogo,yasisitiza usalama Migodini